Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Masinde Bwire, amesema kuwa Kamisheni hiyo haitaendelea kushuhudia vifo vya watu vinavyotokea katika Ziwa Victoria kutokana na upungufu wa vifaa vya uokozi na miundombinu duni ambayo kwa sasa inaboreshwa.
Dkt. Bwire alitoa kauli hiyo katika Kijiji cha Igundu alipofika kutoa pole kwa vifo vya watu sita waliopoteza maisha baada ya ajali ya kuzama katika Ziwa Victoria. Watu hao walikuwa wakitoka Kijiji cha Mwiruruma baada ya kuhudhuria sherehe ya harusi mnamo Septemba 15, 2024.
Mbali na kutoa pole, Dkt. Bwire alikabidhi vifaa vya uokozi kwa kijiji hicho, vifaa ambavyo vitatumika wakati wa kuvuka maji kuelekea upande mwingine wa kijiji.
“Haya majaketi ya uokozi myatumie vizuri, yatabaki hapa kwenye serikali ya kijiji na kata. Mkitumia, hakikisheni mnayarejesha. Mkitumia vifaa vya uokozi, mtakuwa salama na hivyo tutapunguza vifo katika maeneo haya,” alisema Dkt. Bwire.
Aidha, Dkt. Bwire ameagiza kutungwa kwa sheria ndogo zitakazozuia matumizi ya vyombo visivyo rasmi vya usafiri na kusafiri kiholela majini ili kupunguza ajali na vifo visivyo vya lazima.