Meneja Msaidizi wa Mawasiliano BoT, Bi. Noves Mosses katika akimsikiliza Bw. Ignas Athanas Inyasi
Afisa Mtandaji Mkuu wa kampuni ya Blue Coast Co. Ltd wakati akiipongeza BoT alipotembelea katika banda la Benki hiyo maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
Meneja Msaidizi wa Mawasiliano BoT, Bi. Noves Mosses katika akimkabidhi zawadi ya vipeperushi vyenye jumbe mbalimbali za BoT Bw. Ignas Athanas Inyasi Afisa Mtandaji Mkuu wa kampuni ya Blue Coast Co. Ltd wakati alipotembelea katika banda la Benki hiyo katika maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
………………
Bw. Ignas Athanas Inyasi
Afisa Mtandaji Mkuu wa kampuni ya Blue Coast Co. Ltd ameipongeza Serikali ya Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuruhusu ununuzi wa dhahabu kufanywa na benki hiyo kuu. Nyasi, ambaye kampuni yake inasafirisha wafanyakazi wa migodini na kusambaza mafuta kwa migodi, amesema kuwa hatua hii ni muhimu kwani Watanzania ndio wachimbaji wa dhahabu na hivyo wanapaswa kufaidika na rasilimali za nchi yao.
Akizungumza alipotembelea banda la BoT katika maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kwenye viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita, Nyasi alisema: “Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kufanya na kwa mazingira mazuri ambayo Rais Samia ameyaweka ili dhahabu yetu ihifadhiwe Benki Kuu. Sisi wenyewe ndio wachimbaji, hivyo ni haki dhahabu yetu kuhifadhiwa na kusimamiwa na taasisi za nyumbani.”
Aidha, Nyasi alitoa wito kwa Benki Kuu kujenga tawi mjini Geita kutokana na umuhimu wa mji huo katika sekta ya madini. “Geita ina wachimbaji wengi na migodi mingi ya dhahabu, hivyo kuwepo kwa tawi la BoT litasaidia sana katika usimamizi na ukusanyaji wa dhahabu,” alieleza Nyasi.
Pia, alitoa shukrani kwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthonia Mavunde, na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira mazuri kwa wachimbaji wa madini. Nyasi alisisitiza kuwa maboresho yanayoonekana kwenye maonesho hayo ni ishara ya kuimarika kwa sekta ya madini nchini.
“Maboresho tunayoyaona sasa, hata kwenye mabanda ya maonesho, yanaonesha wazi kuwa tumepiga hatua kubwa. Wachimbaji wenzangu, ni muhimu tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha sekta hii na kuboresha uchumi wa nchi yetu,” aliongeza Nyasi.
Mwisho, aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Geita kwa kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika katika mazingira mazuri na kuimarisha uwekezaji, hasa katika sekta ya dhahabu.