Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania{TCRA} Kanda ya Kaskazini imeanzisha kampeni ijulikanayo kama “Ni Rahisi Sana ” inayolenga kuwahimiza watanzania wote kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni kwani uwepo wa mazingira salama mtandaoni yatawezesha kufikia malengo ya uchumi wa Kidijiti.
Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini,Mhandisi Francis Mihayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha .
Aidha amefafanua kuwa , katika wakati tuliopo sasa wa kidigitali matumizi ya teknolojia yamekua yakiongezeka kwa kasi na ni muhimu sana katika maisha ya kila siku .
Mhandisi Mihayo amesema watu wengi nchini Tamzania hawana ujuzi wa kutosha wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii pamoja na namna ya kulinda usalama wao mtandaoni jambo linalowafanya kuwa hatarini kwa mashambulizi ,ulaghai wa mtandaoni na pia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Amesema kufuatia hali hiyo TCRA kupitia kitengo cha mawasiliano na mahusiano ya Umma {CPRU} inatambua umuhimu wa kukuza elimu ya kidigitali na kuhamashisha juu ya fursa zilizopo kwa matumizi sahihi mtandao kwa wananchi wote kushiriki kwa usalama kiuchumi na kisiasa hasa katika kipindi cha chaguzi mbalimbali nchini.
Mhandisi Mihayo amesema TCRA inaungana na Dunia katika kuadhimisha mwezi wa elimu ya usalama mtandaoni ambayo huadhimishwa kila mwaka mwezi oktoba na kitaifa ilizinduliwa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Jabir Bakari kwa uzinduzi kabambe uliojulikana kwa jina la ‘’Ni rahisi sana’’ na kwa kanda ya kaskazini imezinduliwa na meneja wa Mamlaka hiyo.
Amesema katika kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao watanzania wanapaswa kuwa makini na taarifa za mitandaoni kwani baadhi ya watu watatumia mitandao hiyo kutoa taarifa feki na kuzua taharuki hivyo wanapaswa kuwa makini na hilo ili kujiepusha na hilo.
Meneja amesema TCRA imekuwa ikitoa elimu katika maeneo mbalimbali ya wazi kwa miaka mingi ingawa utoaji wa elimu umeendelea kuwa endelevu wakati wote na mabadiliko ya kasi ya teknolojia yamekua yakienda sambamba na ongezeko la vitendo vya ulaghai mitandaoni,ambapo wahusika wamekua wakibuni mbinu mpya kila wakati na kusababisha elimu ya usalama iwe endelevu.
Amefafanua kuwa , kampeni hiyo inalenga kuwapa watu maarifa muhimu ya kidijitali yanayohusu usalama mtandaoni,kuongeza uelewa juu ya jinsi TCRA inavyosaidia bunifu mbalimbali zinazohusu TEHAMA,kuongeza uelewa juu ya kuripoti vitendo vya ulaghai na kukomesha kueneza habari za uongo kwa jamii na kuthamini wateja na wadau wengine nchini.
Amefafanua zaidi kuwa, kampeni hii italenga zaidi watoto,vijana na Wazee wakiwemo watu wenye mahitaji maalum,huku akiwatangazia mashirika au mashirika ya biashara, mashirika yasiuo ya faida na wanafunzi ,wamiliki wa biashara, watoa maamuzi ,waliopewa leseni na TCRA na mashirika ya kitaalamu .