Mkuu wa wilaya ya Kalambo Dkt Lazaro Komba wakati akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Rukwa katika Baraza la uwezeshaji Wananchi kiuchumi
………………
Na Neema Mtuka
Rukwa. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo mkoani humo kwa lengo la kujiinua kiuchumi na kuongeza kipato.
Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa, leo tarehe 9 Oktoba 2024, wakati akiwasilisha mada kwa viongozi wa Mkoa wa Rukwa wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Idara.
Bi. Issa amesema kuwa Programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) inajihusisha na uwezeshaji wa wanawake, vijana, na makundi maalum katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa 5 ya Visiwa vya Zanzibar.
“Kupitia IMASA, wanawake, vijana, na makundi maalum watawezeshwa ili kuimarisha uchumi wao,” alifafanua.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Charles Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dkt. Lazaro Komba, alisema kuwa Mkoa wa Rukwa utaitekeleza programu hiyo kwa vitendo.
Dkt. Komba alisema kuwa jumla ya wakulima 12,000 wamenufaika na mbolea za ruzuku kupitia uwezeshaji uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, aliongeza kuwa lengo la programu hiyo inayoratibiwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ni kuwafikia zaidi ya wananchi 62,000 wa Tanzania Bara.
Sambamba na hayo, Dkt. Komba alisema kuwa kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali itahakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja ili kujiajiri na kuwaajiri wengine.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Adriana Kasambala, wamewataka waratibu wa ngazi za mikoa kuhakikisha uwezeshaji huo unawafikia walengwa bila upendeleo.
Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa inayojenga vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi, hivyo kufungua milango kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali ili kujiinua kiuchumi.