Wataalam wa idara ya afya manispaa ya Ilemela wameshauriwa kuwafikia wananchi kwaajili ya kuwapa elimu ya umuhimu wa bima ya afya ili waweze kuepukana na gharama kubwa wakati wa matibabu
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa mkutano wake wa hadhara katika viwanja vya Kangae ‘B’ kata ya Nyakato ambapo amesema kuwa ipo haja kwa wananchi kuelewa kwa kina juu ya bima ili iwe rahisi kukata
‘.. Ni ngumu sana hawa wananchi kukata bima kama hawana uelewa wa kutosha kuwa bima ina faida gani kwao, Bahati nzuri hata Sisi wawakilishi wao tumeshapitisha sheria ya bima lakini hili halipaswi kuishia katani tu au wilayani, mtenge muda muwafikie wananchi ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amewataka wananchi wa kata hiyo kuwa wavumilivu kutokana na kero ya changamoto za barabara kwa kuwa manispaa ya Ilemela imeweka mkakati wa ununuzi wa vifaa vipya vya ujenzi wa barabara ili kurekebisha barabara za mitaa
Kwa upande wake muwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Jeremiah Lugembe mbali na kumpongeza mbunge huyo kwa kazi nzuri anazozifanya amewahakikishia viongozi wa makundi mbalimbali yanayopatikana ndani ya manispaa hiyo ikiwemo bodaboda ushirikiano na kuwataka kutumia fursa za kujikwamua kiuchumi zilizopo
Lilian Chiguma ni mwakilishi wa mganga mkuu wa wilaya ya Ilemela ambapo amesema kuwa Serikali imechukua juhudi kubwa katika kuboresha sekta ya afya hivyo kuwaasa wananchi kuiunga mkono na kutumia fursa hiyo kujiandikisha katika bima za afya ili kuepuka gharama wakati wa matibabu
Nae Josephat Masunga ambae ni afisa uthamini wa manispaa ya Ilemela amewahakikishia wananchi waliovunjiwa Nyumba zao na muwekezaji kuwa Serikali italifuatilia suala hilo pamoja na kuhakikisha haki na stahiki zao zinapatikana
Silvanus Manija na Nusra Yahya Ramadhan ni wananchi wa mtaa wa Kangae ‘B’ ambapo licha ya kumpongeza mbunge wao na Serikali kwa kazi kubwa iliyofanyika wamelalamikia ubovu wa barabara za mtaa huo na kero ya ukosefu wa maji safi na salama kwa uhakika