Na. Majid Abdulkarim, Mlele
Timu ya Madaktari bingwa wa Mama Samia iliopo Wilaya ya Mlele mkoani Katavi leo Oktoba, 2024 imetoa wito kwa Timu ya usimamizi wa shughuli za afya Wilaya ya Mlele (CHMT) kuwa na ushirikiano na Hospitali ya Wilaya ili kuongeza kasi ya utendaji kazi katika kuwahudumia wananchi.
Wito huo umetolewa na Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Tatu Seif Mbotoni ambaye pia nikiongozi wa Timu ya madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Wilaya ya Mlele.
“Timu ya CHMT wakifanya usimamizi wao kwa karibu na uongozi wa Hospitali itasaidia wananchi kupata huduma bora za afya na kuhakikisha mahitaji muhimu ya Hospitali yanapatikana kwa wakati na wananchi wananufahika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yao”, ameeleza Dkt. Tatu
Dkt. Tatu ameongeza kuwa CHMT wakitimiza wajibu wao ipasavyo itasaidia ubora wa huduma katika hospitali na kupunguza rufaa sisizo za lazima kwani mahitaji yote muhimu ya kutolea huduma bora yatakuwa rafiki kwa mtoa huduma pamoja na mwananchi anayefata huduma za afya.
Amesema kuwa wananchi wengi wamejitokeza kupata huduma za kibingwa na bingwa bobezi kwani walikuwa na uhitaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa kinywa na Meno kutoka hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya amesema kuwa ujio wa kambi yao imekuwa chachu ya kuongeza mapato ya hospitali kutokana na kuongezeka kwa baadhi ya huduma za kibingwa ambazo zilikuwa hazipatikani hospitalini hapo.
“Awali walikuwa wanaona wagonjwa nane mpaka kumi kwa wiki katika kitengo cha maneno lakini ujio wa madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan tumefanikiwa kuona wagonjwa 10 mpaka 20 kwa siku”, ameeleza Dkt. Manyaka
Dkt.Manyaka amesema kuwa kwa mafanikio hayo yaliojitokeza kwa muda mfupi ni chachu na tija ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusimika vifaa vya kisasa, usambazaji dawa na vitendanishi kwa wakati ili wananchi wa ngazi ya msingi waweze kupata huduma bora kwa wakati.