-Asema ni mapumziko ya kitaifa, ili wananchi washiriki kupiga kura kikamilifu .
-Asisitiza kila mwenye sifa ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitangaza 27 Novemba mwaka huu, kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa ili wananchi washiriki kikamilifu kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa.
Rais Dkt. Samia ametangaza hivyo leo tarehe 11 Oktoba 2024, alipokuwa akizungumza na Watanzania, mara baada ya kuzindua zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Wakaazi kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Rais Dkt. Samia ambaye amejiandikisha katika Daftari la Wakaazi wa Kitongoji cha Sokoine, Chamwino Mkoani Dodoma, amesema kila Mtanzania mwenye sifa akajiandikishe kuwa mpiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kusisitiza umuhimu wa kutofautisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, linalotumika kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na Daftari la Wakaazi linalotumika uchaguzi wa Novemba 27, 2024.
“Kuna ubabaifu unajitokeza wengine wanahisi wakijiandikisha kwenye daftari la Tume Huru ya Uchaguzi haina haja kujiandikisha huku tena hapana. Tunajiandikisha kule kwa ajili ya Uchaguzi wa mwakani, lakini hapa kwenye eneo lako unachagua mwenyekiti wako wa kitongoji na kamati yake na viongozi wengine…ni daftari jingine kabisa,” amesema Dkt. Samia.
Rais Dkt Samia amesema kuanzia leo tarehe 11 hadi 20 Oktoba, ni siku za kujiandikisha kwenye Daftari la Wakaazi, hivyo watu wajitokeze kwa wingi kuandikishwa kuwa wapiga kura, akiongeza kuwa kila aliyefikisha miaka 21, mwanamke au mwanamme, yuko mbele kwenye shughuli za maendeleo ama ana uhusiano mzuri na watu katika jamii, kujitokeza kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Serikali ya mtaa.