*Afanikiwa kuishawishi Taasisi ya GTK kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Madini Dar Es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini Finland Oktoba 10, 2024 kwa kukutana na viongozi wa kampuni za biashara na taasisi zinazosimamia biashara na uwekezaji nchini Finland.
Lengo la mikutano hiyo lilikuwa ni kuwaeleza viongozi wa taaasisi hizo hatua ambazo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na fursa zinazopatikana nchini Tanzania.
Wakati wa kikao chake na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Finland (Geological Survey of Finland-GTK), Bw. Kimmo Tiiiikainen, Mhe. Waziri aliishawishi taasisi hiyo ije kuwekeza Tanzania hususan katika eneo la utafiti kwa kuwa ni asilimia sita tu ya miamba ya Tanzania ndiyo imefanyiwa utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mhe. Waziri ameialika taasisi hiyo kushiriki Mkutano wa 5 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwerzi Novemba 2024 ili ijionee yenyewe fursa lukuki za sekta ya madini zinazopatikana Tanzania.
Taasisi hiyo imekubali mwaliko huo na Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden ambao unawakilisha pia Finland umeagizwa kuratibu ushiriki wa taasisi hiyo katika mkutano huo muhimu.
Aidha, Mhe. Waziri Kombo alikutana na Wakurugenzi Waandamizi wa Taasisi ya Business Finland wakiongozwa na Bw. Jusa Susia. Taasisi hiyo ni ya Serikali ya Finland ambayo moja ya jukumu lake kubwa ni kuvutia biashara, utalii uwekezaji wa nje na kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za ubunifu na ugunduzi.
Wakati wa kikao na taasisi hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Uratibu wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE) ziliwasilisha mada kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Kufuatia mada hizo pande mbili zimekubaliana kuandaa Mkutano wa Wafanyabiashara wa Finland na Tanzania haraka iwezekanavyo ili utoe fursa kwa kampuni za Finland kujua zaidi kuhusu fursa za Tanzania.
Mhe. Waziri Kombo amekutana pia na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Finland (Finnfund), Bw. Jaakko Kangasniemi. Mfuko huo moja ya malengo yake ni kutoa fedha kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ambayo itasaidia kutatua changamoto zinazozikabili ulimwengu kama vile uhaba wa ajira na mabadiliko ya tabianchi.
Pande mbili zilikubaliana uongozi wa Finnfund ujiwekee utaratibu wa kutembelea Tanzania ili pamoja na mambo mengine, Watanzania waijue taasisi hiyo kwa lengo la kuchangamkia fursa wanazozitoa
Mhe. Waziri alihitimisha ratiba yake kwa kukutana na Watanzania wanaoishi Finland. Mhe. Waziri pamoja na mambo mengine, aliwaeleza kuhusu mchakato wa hadhi maalum kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni unavyoendelea. Alisema hatma ya mchakato huo ipo kwao wenyewe kwa kujitokeza kwa wingi kujisajili ili Bunge liweze kujua idadi yao ili ione umuhimu wa kupitisha sheria hiyo.
Aliendelea kueleza kuwa zoezi la kujiandikisha lina dhamira njema na wala Serikali haina agenda ya siri katika suala hilo isipokuwa inahitaji kujua takwimu za Watanzania wanaoishi ughaibuni ili ione umuhimu wa kupitisha sheria hiyo.
Ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya Watanzania wanaoishi ughaibuni kuhamasisha wanachama wao kujisajili kupitia Balozi za Tanzania ambazo zimetoa kiunganishi maalum (link) kwa ajili ya kurahisisha zoezi hilo.