Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi,akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 leo Oktoba 12,2024 jijini Dodoma.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi,akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 leo Oktoba 12,2024 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Ndg. Juma Ali Khatibu,akizungumza wakati wa mafunzo kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 leo Oktoba 12,2024 jijini Dodoma.
Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Siasa wakimsikiliza Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi (hayupo pichani), wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 leo Oktoba 12,2024 jijini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Vyama vya Siasa nchini vimekumbushwa kufanya siasa za kistaarabu wakati wote wa kampeni ili kulinda amani na umoja wa taifa.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Mhe. Jaji Francis Mutungi ametoa rai hiyo leo Oktoba 12, 2024 jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa vyama hivyo yaliyotolewa na ofisi hiyo kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Mhe. Jaji Mutungi amesema kuwa vyama vya siasa ni wadau muhimu katika siasa za nchi na kwamba uchaguzi hauwezi kufanikiwa endapo hapatakuwa na ushiriki wa vyama hivyo kwani wagombea wote lazima wadhaminiwe na vyama vyao.
Vile vile, ameeleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatumiwa na vyama hivyo kuweka misingi imara kuelekea uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025, hivyo uchaguzi huu ni muhimu kwao.
“Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa vyama vya siasa katika uchaguzi na umuhimu wa kuendelea kuwa na taifa moja linalotunza amani kama tunu yetu adhimu, tumeandaa mafunzo haya ili kuwakumbusha kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kipindi chote cha uchaguzi na kujiepusha na matumizi ya lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi yetu”, amesema Jaji Mutungi.
Amevisisitiza vyama hivyo kuwa amani na umoja wa taifa ni muhimu zaidi kuliko uchaguzi kwani amani ikikosekana hata fursa ya kushiriki uchaguzi haitakuwepo. Ametoa rai kwao kuwa mabalozi wa amani ya taifa la Tanzania.