Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaji Dk,Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi mara baada ya kuwasili katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akijumuika na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
Mhadhiri kutoka Nchi ya Uingereza Sheikh Ali Hammud akitoa mada kuhusiana na Amani ni Msingi wa Maendeleo na kujenga Pepo na Nchi katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
Mhadhiri kutoka Nchi ya Australia Sheikh Wael Ibrahim akitoa mada kuhusiana na Heshima na kujenga Umoja katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
Mhadhiri kutoka Nchi ya Misri Sheikh Mohamad Salah akitoa mada kuhusiana na Mafanikio ya Dunia na Akhera katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
Mufti Menki kutoka Zimbabwe akitoa mada kuhusiana na Umuhimu wa Swala na Heshima Umoja na Mshikamano katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa lililofanyika katika Uwanja Aman Komplex Zanzibar.
ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ni nchi salama kwa utalii wa mikutano na makongamano ya kimataifa.
Al hajj Dk. Mwinyi ameyasema hayo kwenye Kongamano la kwanza la Kiislam la kimataifa lililowakutanisha pamoja Mashehe mbalimbali kutoka mataifa 18 duniani hapo viwanja vya “New Amani Complex, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dk. Mwinyi amesema, Zanzibar ina fursa kubwa ya kukuza utalii wa maadili “Halal Tourism” kama chanzo cha mapato na ajira kwa watu wake, kupitia kongamano hilo la Kiislamu la kimataifa, limetoa mwangaza kwa nchi kama sehemu ya utalii wa Maadili hasa kwa wageni wanakuja kuitembelea sio tu kujifunza dini lakini kufurahia uzuri wa mandhari na haiba ya nchi, mila, silka, utamaduni na ukarimu wa watu wake.
Akizungumzia faida za kongamano hilo, Al hajj Dk. Mwinyi amebainisha kuwa haziko za kiimani pekee, bali pia kuna manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Taifa.
Pia, ameeleza mafanikio ya tukio hilo muhimu kwa Zanzibar, ni ufunguo adhimu wa kuitangaza kwa utalii wa maadili “Halal Tourism”, ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wanakuja kushiriki mikusanyiko ya kidini na matukio yenye uhusiano na tamaduni za dini.
Aidha, amesema ni jambo la kujivunia na kumshukuru Mwenyezi Mungu kuona wageni wengi kutoka mataifa tofauti duniani wameungana kupitia mitandao ya jamii kuangalia moja kwa moja Kongamano hilo muhimu.
Al hajj Dk. Mwinyi amewahakikishia Wananchi wa Zanzibar kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mikusanyiko kama hiyo na kuunga mkono jitihada za Taasisi binafsi za zile za Serikali ikiwemo kukuza Uchumi na maadili ya nchi ili kupatikane jamii yenye maadili na kuiweka nchi kwenye hadhi ya utalii wa maadili ambao hivi sasa umeshika kasi duniani.
Hata hivyo, ameiasa jamii kuendelea kudumisha maadili kwenye maisha yao ya kila siku, ili kujenga taifa lenye maelewano, amani, heshima na ushirikiano kwa wote. Hatua hiyo ina mchango muhimu katika kupatikana kwa mafanikio yetu hapa Duniani na kesho mbele ya haki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, amesifu amani iliopo nchini na kueleza utulivu wa watu wake kutokana na ukarimu na maadili haya walivyoonesha kwenye kongamano hilo.
Akihadhir mbele ya zaidi ya waumini wa Kiislam na Waananchi wa Zanzibar 20,000 waliofika viwanja vya “New Amani Complex kumshuhudia, Mufti Mkuu wa Zimbabwe, Mufti Ismael Menki amasema maendeleo kwa taifa lolote duniani hayatimii pasi na kuwepo usatawi wa amani na usalama kwa nchi na watu wake kwa kuendeleza, kudumisha Umoja, upendo na kuheshimiana miongoni mwa jamii.
Mufti Menki amesisitiza mshikamano miongoni mwa jamii na kuwasihi waendelee kufungamana kwa Imani, heshima na upendo sio kufarakana kwa tofauti za mitazamo ya dini na Siasa.
Pia, amewasisitiza waislamu kuzingatia zaidi utulivu wanapokuwa kwenye sala zao kwani kufanya hivyo ni kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu (S.W), vile vile amepongeza maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar akitoa ushuhuda wa tofauti ilivyosasa na miaka 10 iliyopita ikiwa mara ya kwanza kufika Zanzibar wakati huo.
Wakizungumza kwenye Kongamano hilo, Sheikh Ali Hamuuda Ali kutoka Uingereza, Sheikh Wael Ibrahim kutoka Australia na Dk. Muhammad Salah, Sheikh kutoka Misri, wamesisitiza Waananchi wa Zanzibar kuendelea kutunza Amani na usalama kwa usatawi wa nchi yao hasa katika kuzifikia ndoto za Maendeleo ya Taifa lao.
Wameeleza uwepo wa amani na utulivu wa nchi husaidia hufanikisha mazuri yasiyowezekana, kuwezekana kwa usatawi mzima wa jamii.
Aidha, masheikh hao pia wamehimiza kuhusu kuzikimbia dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kutofanya matendo yatakayomkosea Allah (S.W) pamoja na kujiepusha na anasa zinazomchukiza, Mwenyezi Mungu.
Eneo jengine waliloligusia masheikh hao ni kusisitiza waislamu kusalimiana kwa upendo na kushirikiana kwa wen ana hata wasiokua waislam ili kujenga jamii moja yenye usawa, upendo, kusheshimiana kwenye kujenga maendeleo ya nchi yao pamoja na kuwahimiza kudukisha sala za usiku katika kujitakasa na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (S.W) ili kujiepusha na maovu yanayotokana na sheitwani na kujitakasa kwa Allah (S.W).
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya “Light upon light” (Noor alaan Noor) Sheikh Nadir Mahfoudh, amemshukuru Rais Al haji Dk. Mwinyi na Serikali kupitia Ofisi ya Makamo wa pili wa Rais na Ofisi ya Utawala bora chini ya uratibu wa Ofisi ya Muft wa Zanzibar kwq kukusimamia kongamano hilo hadi kufanikiwa kwake.
Hii ni mara ya kwanza kwa historia ya Zanzibar kufanya kongamano kubwa la kidini la kimataifa lililojumuisha wahadhiri na mashekhe mbalimbali maarufu kutoka nje ya nchi.
Aidha, Kongamano hilo liliandaliwa na kuratibiwa na Taasisi ya Light upon light kwa ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, lililofuatiliwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari vya ndani na mitandao ya jamii liliangaliwa na zaidi ya watu 1.3 bilioni duniani kote.
@@@@@@@@@@@@ @@@@@@@@@@@@@ @@@@@@@@@@@
Wakati huo huo, Mufti Mkuu wa Zimbabwe Mufti Ismael Menki, akiwaongoza Sheikh Ali Hamuuda Ali wa Uingereza, Sheikh Wael Ibrahim wa Australia, Dk. Muhammad Salah, Sheikh kutoka Misri na Ust. Munir Amour, Mzanzibari anaeeneza nuru ya elimu ya Qur’an kupitia taasisi ya “Light Upon Light” nchini Uingereza walifika Ikulu ya Zanzibar kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi kumshukuru kwa mapokezi ya heshima waliopokewa na Serikali na Wananchi wa Zanzibar na kumueleza kufarajika kwao kwa upendo mkubwa walioupata kutoka wa Wazanzibari.