Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma Jonas Mbunda kulia,akimsikiliza Afisa Mwandikishaji wa Daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa Witness Makoy aliyevaa kapelo, alipofika kwa ajili ya kujiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura katika kituo cha Ruhuwiko B Mjini Mbinga,kushoto Msimamizi Msaidizi wa kituo hicho Florida Chuwa.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma Jonas Mbunda kulia,akijiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura katika kituo cha Ruhuwiki B Mbinga mjini kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika hivi karibuni,aliyesimama ni Msimamizi Msaidizi wa kituo cha Wapiga kura Ruhuwiko B Florida Chuwa.
Mkazi wa mtaa wa Ruhuwiko B kata ya Ruhuwiko Halmashauri ya Mji Mbinga Noela Shija kulia,akijiandikisha katika Daftari la Orodha la wapiga kura katika kituo cha Ruhuwiko B kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Tarehe 27 mwezi ujao.
Na Mwandishi Maalum,
Mbinga
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini mkoani Ruvuma Jonas Mbunda,amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura ili wapate haki ya kushiriki na kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika hivi karibuni nchini kote.
Mbunda,amesema hayo baada ya kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura katika kituo cha Ruhuwiko B kata ya Ruhuwiko Mbinga mjini.
Alisema,zoezi la kujiandikisha katika Daftari la Wapiga kura lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania kwa kuwa linatoa nafasi kwa kila Mtu mwenye sifa kuchagua kiongozi anayemtaka katika mtaa,kitongoji na kijiji.
Alisema,viongozi hao ni muhimu kwa kuwa wanatakiwa kwenda kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi ili kuwaleta maendeleo na kusimamia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao.
Mbunda alieleza kuwa,uchaguzi wa Serikali za mitaa ni daraja ambalo litawasaidia Watanzania kushiriki vyema katika uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka 2025.
“Wito wangu kwa wananchi wa Jimbo la Mbinga mjini kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kupata nafasi ya kikatiba ya kuchagua viongozi tunaowataka katika maeneo yetu”alisema Mbunda.
Aidha, amewaomba wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaofaa ambao watawaletea maendeleo na kuepuka kuchagua viongozi kwa misingi ya ukabila na udini.
Kwa upande wake Afisa Mwandikishaji wa kituo cha Ruhuwiko B Witness Makoy alisema,zoezi hilo linaendelea vizuri huku idadi kubwa ya wananchi wakiendelea kujitokeza kujiandikisha.
Aliongeza kuwa,hali hiyo imetokana na hamasa kubwa iliyofanyika kupita mtaa kwa mtaa ili kuwakumbusha na kuwahimiza wananchi kwenda kupata haki yao kabla siku ya uchaguzi wa Serikali za mitaa Tarehe 27 Mwezi Novemba.
Kwa mujibu wa Makoy ni kwamba,mwananchi anatakiwa kufika kwenye kituo akiwa na kadi za Bima ya afya,Nida,kadi ya mpiga kura,leseni ya udereva na vyeti kwa wanafunzi waliofikisha umri wa miaka 18.
Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Ruhuwiko B kata ya Ruhuwiko Noela Shija,ameipongeza Serikali kwa kuleta Daftari la wapiga kura kwani litasaidia baadhi ya wananchi waliopoteza kadi za mpiga kura zilizotumika katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Alisema,zoezi hilo litasaidia wananchi kupata haki ya kuchagua viongozi wanaowapenda na ambao watawaletea maendeleo kwa kushirikiana na Serikali yao iliyopo madarakani.