Mkurugezi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah akiwasilisha taarifa ya Utendaji na Mikakati ya NHC kwa viongozi wa Wilaya ya Ilala kuanzi ngazi ya Mtaa leo Oktoba 13, 2024 jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imefanikiwa kuongeza mapato yake kwa asilimia 47 kwa kipindi cha miaka mitano kutoka shilingi bilioni 125 kwa mwaka hadi kufikia shilingi bilioni 184.
Akizungumza leo Oktoba 13, 2024 jijini Dar es Salaam na viongozi wa Wilaya ya Ilala kuanzia ngazi ya Mtaa wakati akiwasilisha taarifa ya Utendaji na Mikakati ya NHC, Mkurugezi Mtendaji wa NHC Bw. Hamad Abdallah, amesema kuwa katika kipindi cha miaka hiyo mitano serikali imefanikiwa kupata faida ya shilingi bilioni 199.3 sawa na ukuaji wa asilimia 30.3.
Bw. Abdallah amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024 serikali ilipata faida ya kabla ya kodi shilling bilioni 42. 25 sawa na asilimia 147 ya lengo kwa hesabu ambazo bado hazijakaguliwa na mkaguzi mkuu wa serikali (CAG).
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano hadi kufikia sasa shirika iliweza kulipa kodi mbalimbali pamoja na gawio serikalini zinazofikia shilingi bilioni 134.55.
“Thamani ya mali za shirika hadi kufikia juni 2024 ilikuwa shilingi trilioni 5.16 ukilinganisha na mwaka uliopita ilikuwa trilioni 5.04” amesema Bw. Abdallah.
Bw. Abdallah amesema kuwa shirika linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukandarasi na ushauri elekezi, ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu na kati, uboreshaji wa miji kwa kuvunja majengo ya zamani na kujenga mapya.
Miradi mengine ni upangaji wa miji na uendelezaji vitovu vya miji, uendelezaji wa miji kwa njia ya ubia (Mkazi, Biashara na Viwanda).
Amefafanua kwa katika miradi ya ukandarasi shirika linatekeleza miradi nane ya majengo ya serikali Mtumba yenye thamani ya shilingi bilioni 186 inayotarajiwa kukamilika Januari 31, 2025.
Miradi mengine ni ujenzi wa shule maalumu Mbuye Chato ambao umegharimu shilingi bilioni 5.5 na umefikia asilimia 96 pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kwangwa Musoma ambao umegharimu shilingi bilioni 15.1 na umefikia asilimia 100.
Ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje, Hospitali ya Ligula Mtwara ambao umegharimu shilingi bilioni 2.7 na umefikia asilimia 99.
Bw. Abdallah ameeleza kuwa wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme wenye Nyumba 5,000 kwa awamu ambao utagharimu shilingi bilioni 466.
“Katika kutekeleza mradi huu, maandalizi ya ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe unaendelea na umefikia 75, maandalizi ya ujenzi wa 100 jijini Dodoma na nyumba 400 eneo la Mtoni Kijichi yanaendelea kukamilishwa” amesema Bw. Abdallah.