Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dastan Kitandula amesema kuwa Sekta ya Utalii imepiga hatua kubwa kutokana na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuipa kipaumbele Sekta hiyo hali inayochangia kukuza uchumi wa nchi.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Uwekezaji katika Sekta ya Utalii Nchini Tanzania lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam,ikiwa ni sehemu ya onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Kiswahili( S!TE) 2024.
Amesema kuwa kutokana na uwekezaji mzuri wa miundombinu rafiki katika sekta hiyo,imechangia kwa kiasi kikubwa kuwavutia watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza Nchini.
Aidha Kitandula amesema kuwa sekta ya Utalii inaingiza fedha nyingi za kigeni,pamoja na kuchangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa( DGP) hivyo Serikali itaendelea kuweka jitihada za msingi katika kuimarisha uwekezaji kwenye sekta hiyo.
“Sekta ya Utalii inaingiza fedha za kigeni,inatangaza utamaduni,inatoa ajira ,inachangia kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa,na kuleta Maendeleo katika jamii,hivyo serikali inaendelea kuweka miundombinu mizuri ya uwekezaji katika Sekta ya Utalii” amesisitiza Kitandula.
Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasi na Utalii Nkoba Mabula amesema kwamba,kuna fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya utalii nakuwahimiza watu wote wanaohitaji kuwekeza wafike katika Ofisi za mamlaka za uwekezaji ikiwemo Kituo Cha uwekezaji Tanzania( TIC) na Kituo Cha uwekezaji serikali ya Mapinduzi Zanzibar (ZIPA) wapate taratibu hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania( TTB) Ephraim Mafuru amesema kuwa lengo la onesho hilo ni kuwakutanisha Watoa huduma waliopo katika mnyororo wa thamani wa Utalii Ndani na nje ya Nchi ambao watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao za Utalii na kutengeneza Mtandao wa Biashara( Business Network)
Onesho la S!TE linaenda sambamba na Utekelezaji wa sera ya Taifa ya Utalii ya Mwaka 1999 pamoja na mkakati wa kutangaza Utalii Kimataifa ( 2020-2025 ) ambayo imetilia mkazo kutangaza Tanzania kama kivutio Bora cha Utalii Duniani.
The post Sekta ya utalii inachangia kiasi kikubwa katika pato la taifa first appeared on Millard Ayo.