Muungano wa nchi 104 wanachama wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Umoja wa Afrika, umelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kumtangaza Katibu Mkuu Antonio Guterres “kuwa mtu asiyetakikana.”
Kundi hilo limetangaza uungaji mkono mkubwa kwa Guterres hata baada ya marufuku hiyo ya Israel.
Taarifa hiyo imekosoa uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Yisrael Katz na kusema kuwa kumpa Guterres sifa ya “mtu asiyokubalika” kunadhoofisha mamlaka ya Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo imesema mataifa 104 yamethibitisha tena uungaji mkono kamili na imani kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kazi zake.
Nchi zilizotia saini taarifa hiyo pia zimetaka kuheshimiwa uongozi wa Umoja wa Mataifa na kazi zake.
Wanachama 104 wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa pande zote kuepuka vitendo vinavyoweza kudhoofisha jukumu muhimu la Umoja wa Mataifa katika kutatua migogoro na, badala yake, kuunga mkono mipango inayochangia suluhisho la amani na la kudumu la mgogoro wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi).
Hivi karibuni utawala wa kibaguzi wa Israel ulimtangaza Guterres kuwa “mtu asiyetakikakana” na hivyo kumpiga marufuku kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Uamuzi huo ulifuatia matakwa ya Guterres ya kusitishwa mara moja kwa mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati.
The post Umoja wa Afrika walaani hatua ya Israel ya kumpiga marufuku Guterres first appeared on Millard Ayo.