Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kifo cha Baba wa Taifa, wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari Milambo, ambayo hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kufundisha wakati wa uhai wake, wamekabidhi tuzo maalum kwa Nyumba ya Baba wa Taifa. Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa Tuzo ya Mwalimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa AMSHA, Derrick Mlusuri, alieleza kuwa lengo la kuanzisha Tuzo ya Mwalimu ni kutambua mchango mkubwa wa walimu nchini, pamoja na kuwapa heshima waliowahi kutumikia taifa hilo katika nyanja ya elimu. Alisisitiza kuwa kumpa tuzo hayati Mwalimu Nyerere ni ishara ya kuthamini jitihada alizozifanya katika ualimu kabla ya kuingia kwenye siasa. Aliongeza kuwa tuzo hiyo itatolewa kila mwaka kwa walimu waliotoa mchango mkubwa kwa jamii.
“Tunataka kutambua mchango wa walimu. Wengi wao wanakumbana na changamoto nyingi, lakini wametumia muda mwingi kutuelimisha. Leo hii sisi tunaishi maisha mazuri, lakini mara nyingi tunawasahau walimu waliotuwezesha kufika hapa,” alisema Derrick Mlusuri.
Kwa upande wake, Mjumbe wa AMSHA, Abdul Razaq Badru, alisema kuwa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni mtu wa pekee mwenye mchango mkubwa katika historia ya wanafunzi wa Milambo. Aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere ameacha alama kubwa katika elimu na maarifa, ambayo yanaendelea kuwaongoza wanafunzi waliofaidika na juhudi zake.