Ashrack Miraji, Fullshangwe Media – Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Jafari Kubecha, amewahimiza vijana kuwa wazalendo ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kudumisha demokrasia na kushiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali, zikiwemo za mitaa, vijiji na vitongoji.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, DC Kubecha alisema Nyerere alikuwa mfano bora wa demokrasia, hata kufanikisha kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na baadaye kuamua kuachia madaraka, jambo ambalo ni nadra kwa viongozi walioongoza harakati za uhuru wa nchi zao.
Kubecha alitoa kauli hiyo aliposhiriki zoezi la usafi katika Soko la Samaki la Deep Sea, akishirikiana na wananchi katika maadhimisho hayo. Aliwataka vijana wa Tanzania kuendeleza amani, umoja, mshikamano, na kuwa na uzalendo kwa Taifa, ili kumuenzi Nyerere kwa vitendo.
Aliongeza kuwa, katika miaka 25 tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere, vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwa maisha yake, aliyokuwa na utu, busara, na moyo wa kutosheka na madaraka. Sifa hizi ziliweza kumpatia heshima kubwa ndani ya nchi, barani Afrika, na duniani kote.
Pia, DC Kubecha alisisitiza kuwa tunu za taifa ambazo zilianzishwa na Baba wa Taifa zinaendelea kulindwa na marais waliomfuatia, kuanzia Hayati Benjamin Mkapa (awamu ya tatu), Jakaya Kikwete (awamu ya nne), Hayati John Magufuli (awamu ya tano), hadi sasa Rais Samia Suluhu Hassan wa awamu ya sita.