Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka vijana kuwa wazalendo ili kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kudumisha Demokrasia na kushiriki katika chaguzi kwa kupiga kura kwenye chaguzi za mitaa, vijiji na vitongoji.
Amesema Mwalimu Nyerere amekua kiongozi wa kuonesha mfano mzuri wa Demokrasia hata kukubali uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 nchini na kukubali kung’atuka katika madaraka jambo ambalo si lakawaida kwa viongozi waliopigania uhuru wa nchi zao.
Mpogolo ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesma ili kumuenzi Nyerere na kuendelea kumkumbuka ni vema vijana wa Tanzania kudumisha amani, umoja, mshikamano na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Ameongeza kuwa miaka 25 ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere kilichotokea tarehe 14 ya mwezi 10 mwaka 1999 katika hospitali ya mtakatifu thomas nchini uingereza alikokua anapatiwa matibabu ya maradhi yaliyokua yanamsumbua ni majonzi kwa Taifa.
Ameeleza miaka 25 ya kifo cha Mwalimu vijana wanatakiwa kujifunza maisha ya mwalimu Nyerere aliyependa Utu, kujifunza na kutosheka katika madaraka hali iliyomjengea heshima ya kisiasa nchini, barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Amesisitiza kitendo cha mwalimu Nyerere kuaminiwa na wazee na chama cha Tanu kuongoza Watanganyika kutafuta Uhuru ni kutokana na heshima, busara na unyenyekevu licha ya elimu yake alikubali kutumwa kusaidia nchi yake.
Mpogolo amesema Hayati Mwalimu Nyerere amekua na mchango mkubwa kuhakikisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar unafanikiwa kwa kushirikiana na aliyekua Rais wa Zanzibar Hayati Shekhe Abeid Amani Karume, muungano ambao hadi sasa unaendelea kudumishwa.
Licha ya ndoto yake ya kutamani Bara lote la Afrika linaungana bado Watanzania wanaona mchango wake wa kuunda umoja wa nchi za Afrika mashariki unaendelezwa.
Mpogolo ameeleza alama aliyoacha Mwalimu Nyerere ni kubwa maeneo mbalimbali nje ya Tanzania kwa nchi zilizosaidiwa na Mwalimu Nyerere kupata uhuru ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, Angola na Namibia.
Amebainisha kumbukizi ya miaka 25 ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere watanzania bado wanashuhudia Marais wa awamu zote wakiendelea kulinda tunu za Taifa la Tanzania toka kifo chake kilipotokea kipindi cha awamu ya tatu chini ya hayati Benjamin Mkapa, awamu ya nne ya Jakaya Kikwete, awamu ya tano ya Hayati John Magufuli hadi sasa awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Jambo ambalo Watanzania wataendelea kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere ni kuwacha katika misingi ya umoja, amani, upendo na mshikamano pamoja na kukemea suala la udini, ukabila na ukanda katika Taifa.