NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 18 ya wanafunzi wa kidato cha nne, Shule ya Sekondari ya Somsom iliyopo Kata ya Kibosho Magharibi Halmashauri ya Moshi.
Mbunge aliongozana na viongozi mbalimbali kuelekea maeneo ya shule kujionea mazingira ya shule na miradi ya kilimo, ufugaji na ujenzi wa nyumba ya walimu kupata fursa ya kuona maonyesho ya taaluma kutoka kwa wanafunzi katika masomo ya Kemia, Biolojia, Fizikia na Kilimo.
Katika mahafali hayo Wahitimu, Mwalimu Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa bodi ya shule walisoma risala mbele ya mgeni rasmi ambazo kwa ujumla zilieleza mafanikio na changamoto zinazoikabili Sekondari ya Somsom.
Changamoto zilizotajwa na wanafunzi pamoja na mkuu wa shule ilikuwa ni pamoja na upungufu wa walimu wa hesabu na kiingereza, ukosefu wa maktaba, ukosefu wa bwalo ambapo kwa sasa wanapata chakula madarasani, uchakavu wa miundombinu ikiwemo ofisi ya mwalimu mkuu, wanafunzi wengi kupata mimba, kuchelewa kukamilika maabara, upungufu mkubwa wa madawati na ubovu wa barabara ya kuingia shuleni.
Akiongea na hadhara, Mbunge Ndakidemi alimpongeza Makamu Mwenyekiti wa Bodi na uongozi wa shule kwa usimamizi mzuri, jambo lililosababisha shule kuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma kwenye mitihani ya kidato cha nne.
Mbunge aliishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivoleta maendeleo kwenye sekta ya elimu hapa nchini kwani serikali imewaondolea wazazi mzigo wa kulipa ada kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha sita aliishukuru serikali kwa ujenzi wa madarasa matatu shuleni hapo kupitia mradi wa UVIKO.
Akijibu risala zao, Mbunge alisema kuwa ni muhimu uongozi wa shule ukaendelea kushirikisha wadau wa maendeleo ili waweze kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekondari ya Somsom.
Alilaana kitendo cha kuwarubuni watoto na kuwapa Mimba na kuwaomba wazazi washirikiane na Serikali kuwachukulia hatua wahalifu hawa.
Aliwaomba wadau wote wa maendeleo waliotoa ahadi zao kutekeleza kile walichoahidi, ikiwemo ile ya ukarabati wa barabara ya kuingia shuleni hapo iliyotolewa kwenye mahafali ya mwaka jana.
Mbunge alitoa mchango wake na kuelekeza uende kwenye ukarabati wa ofisi ya mwalimu mkuu huku changamoto zinazohitaji msaada wa Serikali kuu, Mbunge aliahidi kuzipeleka kwenye mamlaka husika.
Kwa moyo wa upendo kwa shule yao, wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne walimwomba mgeni rasmi aendeshe zoezi la kulisha wageni wote waalikwa keki ili wachangie ukarabati wa angalau darasa moja ambapo katika zoezi hilo, zilipatikana shillingi 1,356,500.
Mbunge alihitimisha risala yake kwa kuwapongeza wahitimu, na kuwashukuru wazazi kwa jinsi walivyosaidia watoto wao kufikia mafanikio yao na kugawa vyeti vya kuhitimu kwa wanafunzi 92 na zawadi mbalimbali.