Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuzindua Kitabu cha kitabu maalumu kuhusu historia ya Mwenge wa Uhuru.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi wakati akihitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge ambazo kitaifa zimefanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba tarehe 14 Oktoba, 2024.
Matukio mbalimbali katika kilele cha Maadhimisho ya mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza tarehe 14 Oktoba, 2024.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa maono na fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zinaendelea kuishi, na Taifa la Tanzania linaendelea kujivunia amani, mshikamano na umoja.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa historia ya Mwalimu Nyerere haiwezi kutofautishwa na historia ya Mwenge wa Uhuru, ambayo ni Tunu ya Taifa ambayo Mwalimu Nyerere amewaachia Watanzania.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo wakati wa Kumbukizi ya Miaka 25 ya Kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere na Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba.
Rais Dkt. Samia amewapongeza vijana walioshiriki mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2024 kwa kuzunguka nchi nzima kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Vilevile, ameeleza kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Ndugu Godfrey Eliakim Mzava inayojumuisha changamoto, maombi na ushauri uliotolewa na wananchi kupokelewa na Mwenge wakati wa mbio hizo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa vijana kuendelea kulinda Mwenge wa Uhuru ambayo ni Tunu ya Taifa na kuuenzi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumzia Maonesho ya Wiki ya Vijana, Rais Dkt Samia ametoa pongezi kwa vijana kwa ubunifu, ujuzi, uthubutu na utayari wao walioonesha kupitia kazi zao na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika kuchochea zaidi ubunifu wa vijana, Rais Dkt. Samia ameelekeza Halmashauri zote nchini kununua vifaa vinavyotumika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kufundishia wanafunzi ambavyo vinazalishwa kwa ubora na vijana wabunifu hapahapa nchini.
Rais Dkt. Samia pia amerejea wito wake kwa wananchi kujiandikisha ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa ni kuendana na dhamira ya Uhuru ya kuwawezesha wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe, ikiwemo kwa kuwachagua viongozi wao.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu