Watoto wakifuatilia kwa makini mafunzo ambayo yametolewa na Shirika la Save the Children jijini Dododma ya kujadili mambo ya mabadiliko ya tabia ya nchi sambamba na kuandaa tamko (statemeny) la watoto litakayowasilishwa katika mkutano wa 29 wa Vyama vya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29).
…………………………
Shirika la Save the Children limewakutanisha Watoto kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili mambo ya mabadiliko ya tabia ya nchi na kuandaa tamko (statemeny) la watoto litakayowasilishwa katika mkutano wa 29 wa Vyama vya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29).
Akizungumza jijini Dodoma katika mafunzo ambayo ymewakutanisha watoto hao kwa siku tatu kuanzia tar 11 Octoba hadi Octoba 13 mwaka huu, Afisa Mlinzi wa mtoto Save the Children Innocent Estomih amesema malengo ya kuwakusanya watoto hao ni pamoja na kujifunza sera za kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha amesema kama wadau wa watoto mipango yao ni kuhakikisha mtoto anashirikishwa na kuelezewa namna maamuzi yanavyofanywa katika vitu vinavyoathiri afya na maisha yao.
‘Tumeamua kukaa kwenye nafasi hii kuhakikisha watoto hawa wanafahamu mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa yakiwaathiri kwa namna gani na mpaka mwisho wa mafunzo haya watatoka na ujumbe ambao utakwenda kuwasilishwa kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ambao unatarajiwa kufanyika mji wa Baku, nchini Azerbaijan Novemba mwaka huu”amesema Estomih
Afisa Mlinzi huyo wa mtoto amesema wamekuwa wakichajisha umuhimu wa kuwashirikisha watoto katika masuala yote yanayowahusu ikiwemo namna mabadiliko ya Tabia Nchi yanavyowathiri ili waweze kufahamu maamuzi yanavyofanyika.
Kwa upande wake Mkufunzi mambo ya mabadiliko ya tabia ta nchi Humphrey Mrema amesema wameamua kuongea na watoto hao kwa sababu ni sauti ya leo,baadae na ni sauti yenye nguvu kusaidia dunia kuweza kupata mafanikio.
Amesema wamewafundisha watoto hao kuhusu Mkutano wa COP jambo ambalo wamejifunza na kuelewa fursa mbalimbali zilizopo kwenye mabadiliko ya tabia nchi na namna wanaweza kujenga ujuzi wao kuanzia sasa katika kuyasaidia mataifa yao kukabiliana na chnagamoto hiyo.
Baadhi ya watoto walioshiriki katika mafunzo hayo wameiomba serikali iongeze ushirikishwaji watoto katika masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi kama wanavyofanya Shirika la Save the Children ili waweze kuongeza uelewa mkubwa wa mapambano ya changamoto hiyo.
Wameeleza kuwa ni vyema wazazi wakatumia fursa ya matumizi ya nishati mbadala ili kuepukana na changamoto za kiafya ambazo wanaweza kupitaka kupitia moshi wa nishati chafu.
Pia watoto hao wameiomba serikali kujenga shule katika maeneo salama na siyo katika vyanzo vya maji ambayo itasaidia kutokumbwa na mafuriko yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkutano wa Vyama vya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi hufanyika kila mwaka ambao kwa mwaka huu utakuwa ni mkutano wa 29 tangu kuanzishwa kwake na utafanyikia katika mji wa Baku, nchini Azerbaijan.