Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Ewong’on iliyopo kijiji cha Kambi ya Chokaa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanya mahafali ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Mkuu wa shule ya sekondari Ewong’on William Ombay amesema kuwa wanawashukuru wazazi kwa kuwapa moyo na kuwapongeza kwa kuanza ujenzi wa ukuta unaozunguka shule.
“Wazazi na walezi wametupongeza sana kwa kubadilisha mazingira ya shule,wameona yanavutia sana, hata mhe Diwani siku moja kabla ya mahafali alifurahishwa sana na juhudi za walimu kuboresha mazingira na kuanza ujenzi wa ukuta kuzunguka shule,” amesema.
Mwalimu Ombay meeleza kwamba wote wamesema kuwa watawashirikisha wadau kufanikisha ujenzi huo mapema ili uweze kukamilika.
Mmoja kati ya wahitimu hao, Doreen Nolasco akisoma risala amesema walianza kidato cha kwanza wakiwa wanafunzi 102 wakiwemo wavula 50 na wasichana 52.
“Ila leo tumehitimu wanafunzi 73 wakiwemo wavulana 39 na wasichana 34 kwani wengine wameshindwa kuhitimu kwa kuhama shule na utoro na tunamshukuru Mungu kwa ulinzi wake hadi sisi kuhitimu,” amesema.
Amesema wanaomba kukamilishwa uzio unaozunguka shule ili kuzuia mifugo isiharibu mazingira ya shule na pia wanaomba kupatiwa vifaa vya michezo.
Amesema pia wanaomba kupatiwa vitabu vya ziada ili viwasaidie wanafunzi wanaobaki na wanamshukuru kwa kuitikia mwaliko.
Mhitimu mwingine Erick Sylidion shule ina upungufu wa matundu ya vyoo, vitanda bwenini, viti na meza, uchakavu wa sakafu ya madarasa.
“Elimu tuliyoipata imetujengea msingi mzuri wa kujitambua, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na pia ituwezesha kupata elimu ya mambo mbalimbali kupitia masomo tunayofundishwa hapa shuleni mfano uraia na historia, afya na magonjwa mbalimbali, hali ya hewa na tehama,” amesema.
Amesema wanatoa shukrani zao za dhati kwa walimu wao kwa kuwafundisha na kuwalea kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na wanatoa ahadi ya kuyaenzi yote waliyofundishwa na kuwaasa katika maisha yao.
Hata hivyo, mwakilishi wa Diwani wa kata ya Naisinyai Taiko Kurian Laizer amewaahidi wanafunzi hao kutatua baadhi ya changamoto hizo kwa kushirikiana na serikali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Amewaasa wanafunzi hao kujipanga kwa kuendelea kusoma ipasavyo na kuwasikiliza walimu wao wanayowafundisha kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao ya kuhitimu
elimu ya sekondari.