Na Mwandishi Wetu, Kisarawe
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amelishukuru Shirika la WaterAid, kwa kujenga miundombinu ya vyoo na sehemu za kunawa mikono katika shule 30 na vituo vya afya wilayani humo.
Pia ameahidi kuendeleza na kutunza miundombinu ya kunawa mikono iliyojengwa na Shirika la WaterAid katika kampeni ya kuhamasishaji watu kunawa mikono wilayan humo.
Magoti ametoa pongezi hizo jana katika maadhimisho ya siku ya kunawa mikono iliyofanyika Shule ya Msingi Kazimzumbwi wilayani humo, ambapo siku hiyo huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 15, duniani kote.
Magoti amesema katika kampeni hiyo, shirika hilo limewafanyia mengi wakazi wa Kisarawe ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya vyoo na kunawa mikono katika shule 30 na vituo 15 vya afya, hivyo hawana budi kuvitunza ili viwafae katika kulinda afya za wananchi na wanafunzi.
Amesema muhimu wa kampeni hiyo ni kutoa elimu kwa jamii ukizingatia mkono ndio kila kitu na itawaepusha na magonjwa mbalimbali yakiwamo ya tumbo, macho, kichocho,vkipindupindu, kuhara na magonjwa ya homa ya tumbo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Water Aid, Christina Mhando, amesema lengo kuu la mradi wa unawaji mikono ni kuhamasisha tabia siha kwa wananfunzi na watoa huduma za afya walimu na jamii kwa ujumla.
Akizungumzia maadhimisho hayo, amesema huwa wanatumia siku hiyo kuwashawishi watunga sera watoa maamuzi, wafadhili na wadau mbalimbali umuhimu wa kuwekeza kwenye maji na usafi wa vyoo na kunawa.
Christina amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo asilimia 90 imenufaika kwa wanafunzi kunawa mikono, huku asilimia 12 waliripoti kupata magonjwa ya kuhara katika kipindi cha miaka miwili ukilinganisha na asilimia 35 iliyokuwa ikiripotiwa awali.
Naye Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sungwi, Junita Maiko, amesema katika maadhimisho hayo amejifunza mambo mbalimbali, kubwa umuhimu wa unawaji mikono huku akiahidi kwenda kuwa balozi mzuri kwa jamii inayomzunguka.