Na. Faraja Mbise, DODOMA
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko amekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu mwenendo wa uandikishaji kuwa wanaandikishwa mamluki kwenye orodha ya wapiga kura.
Kanusho hilo alilitoa ofisini kwake alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kufuatia tuhuma zilizotolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kuhusu mwenendo wa uandikishaji orodha ya wapiga kura unaoendelea wakidai kuwa kituo kimoja kiliandikisha watu kinyume na utaratibu.
Dkt. Sagamiko alisema “kutokana na taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii, zinazoelezea kuhusu muenendo wa uandikishaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa bahati mbaya sana taarifa ile inaelezea kuhusu mwenendo mbaya wa uandikishaji.
Baada ya kupitia na kusikiliza kwa makini video ile, nikabaini kwamba tatizo sio mwenendo wa uandikishaji, bali tatizo ni uelewa mdogo juu ya kanuni na miongozo inayotumika katika uendeshaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu 2024”.
Msimamizi huyo alifafanua kuwa wanaoruhusiwa kuandikisha katika orodha ya wapiga kura ni maafisa waandikishaji waliochaguliwa na Msimamizi wa Uchaguzi, kushiriki katika kuandika taarifa za mpiga kura. “Kwenye kituo, nje ya mwandikishaji na wakala wa chama, wapo baadhi ya watu walioruhusiwa kikanuni kama Msimamizi wa Uchaguzi, kuhakikisha anatimiza wajibu wake na kwenda kufanya ukaguzi mwingine. Lakini hakuna mtu mwingine anaeruhusiwa kuwa kwenye kituo cha kujiandikishia” alisisitiza Dkt. Sagamiko.
Msimamizi huyo alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina jumla ya vituo 666 vya kujiandikishia wapiga kura na vyama vya siasa vimeruhusiwa kuweka mawakala wao katika kila kituo. “Kwa sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma tuna jumla ya vituo 666, na nchi yetu tuna vyama vya siasa takribani 19 vyenye usajili wa kudumu na sisi tunaamini vyote hivyo vinashiriki katika uchaguzi huu. Halmashauri tulifuata taratibu zote kuwaarifu vyama kuweza kuweka mawakala wakati huu wa kujiandikisha.
Naomba nichukue nafasi hii kuwataarifu kwamba ni vyama viwili tu vilivyofanikiwa kuweka mawakala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kuweka mawakala 666 katika kila kituo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamefanikiwa kuweka mawakala 55.
Kwa kuwa malalamiko yale yametolewa na viongozi CHADEMA, naomba kutoa taarifa kuwa CHADEMA wamefanikiwa kuweka mawakala katika kata sita, kati ya kata 41 zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Kata hizo ni Kikombo (9), Kikuyu Kaskazini (12), Chamwino (7), Chihanga (4), Ng’hong’onha (19) na Mbabala (4). Lakini kwa bahati mbaya eneo ambalo limeripotiwa matukio kutokea hakuna mawakala wa CHADEMA waliowekwa” alisema Dkt. Sagamiko kwa mshangao.
Msimamizi huyo alivitaka vyama vya siasa kufuata kanuni na miongozo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili uchaguzi uwe wa huru na wa demokrasia. “Nitoe rai kwa viongozi wa vyama vya siasa kutokushiriki katika uvunjifu wa amani katika maeneo yetu ya vituo na wazingatie kanuni na kwa bahati nzuri walishagawiwa kanuni” aliongea kwa msisitizo Dkt. Sagamiko.
Wakati huohuo, aliwataka wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wenye sifa za kujiandikisha kujitokeza na kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ili waweze kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa. Aliwahakikishia kuwa hakuna mtu wa kuwapora haki hiyo.
Aliwakumbusha sifa za kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ni kuwa mtanzania, mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, mkazi wa kijiji, kitongoji au mtaa ambao uchaguzi unafanyika na uwe na akili timamu.
Akiongelea umuhimu wa waandishi wa habari na vyombo vya habari, alisema kuwa ni wadau muhimu katika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi. “Kwakuwa ninyi ni wadau muhimu, mnapaswa kuzielewa kanuni hizi. Naomba niwakabidhi kanuni hizi na ninawaomba mzisome na pale mtu yeyote atakapoitwa kwenye ‘press’, mpitie muongozo wa uchaguzi kabla hamjaenda kutoa taarifa ili muweze kujiridhisha kama huyo mtu ameongea kwa mujibu wa kanuni au la” alisema Dkt. Sagamiko.
Ratiba ya shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa inaonesha kuwa zoezi la uandikishaji katika orodha ya wapiga kura lilianza tarehe 11 Oktoba, 2024 litamalizika tarehe 20 Oktoba, 2024.