Na Pamela Mollel,Arusha
Vijana wanaharakati wa mazingira wameshauri kuwepo kwa mkakati wa kimataifa wa kuliokoa bara la Afrika kutokana na athari za uharibifu wa mazingira yanayochangiwa na mataifa yaliyoendelea.
Wametoa ushauri huo katika mkutano wa Haki ya Mazingira uliowakutanisha vijana kutoka mataifa zaidi ya 100 Duniani, mkoani Arusha uliolenga kujadili mbinu endelevu za kupunguza athari za uharibifu wa wazingira.
Faustine Lusanzu alisema kuwa kuelekea mkutano mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wanaamini viongozi watakaokutana watafanyia kazi ushauri huo hivyo wanatuma sauti zao na huenda mabadiliko ya tabia yakabaki kuwa historia.
Ziada Kassim mwanaharakati wa mazingira alisema kuwa athari za mabadiko ya nchi zinaendana katika maeno mbalimbali hasa Afrika hivyo wanapokutana pamoja wanatoka na majawabu yanayoendana jambo linalosaidia kuleta mabadiliko
Happiness Njile alisema vijana ni kundi linalosambaa kila sekta hivyo athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ni jambo linalowakabili na linahitaji ufumbuzi hivyo wapo katika mkutano huo kuona kila nchi ina athirika vipi na nini kifanyike kuondoka na madhara hayo.
Kwa upande wake Agus Naggio Mratibu wa mkutano wa haki ya mazingira alisema kuwa wanachokifanya ni kuunda nafasi kwa viongozi vijana kutoka kote ulimwenguni kukusanyika na kuchukua hatua za pamoja katika kukabiliana na athari hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa fursa nyingi kwa kadri inavyowezekana kwa vijana ili waweze kurudi katika jumuiya zao na kuendelea kuhamasisha hatua za kuchua kupambana na tabia ya nchi.