Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa masoko katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya ilemela.
Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa soko la samaki Mkuyuni.
Utiaji saini mkataba wa ujenzi wa soko la Kirumba ukiendelea
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya utiaji saini ujenzi wa soko la kirumba na ujenzi wa soko la samaki Mkuyuni uliofanyika Jijini Mwanza.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa masoko
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mh.Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda pamoja na Wenyeviti wa Chama Cha mapinduzi (CCM) kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa ili iweze kukamilika kwa wakati.
Maagizo hayo ameyatoa leo Octoba 16, 2024 kwenye hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa Soko la Kirumba na Barabara ya Kirumba Katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na Soko la samaki Mkuyuni katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia miradi ya uboreshaji Miji Tanzania (TACTIC).
Amesema Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza wanapokwenda kusimamia utekelezaji wa ilani wahakikishe wanakagua miradi hiyo na wanapobaini kunachangamoto zinazoweza kukwamisha miradi kukamilika kwa wakati watoe taarifa kwa wahusika ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Miradi hiyo itagharimu bilioni 22.7 ambapo ujenzi wa soko la samaki Mkuyuni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka sokoni utagharimu bilioni 7.36 na ujenzi wa soko la kirumba pamoja na ujenzi wa barabara za kuzunguka soko (lenye urefu wa km 2.9) utagharimu bilioni 14.71.
Aidha, ameeleza kuwa hakutakuwa na nyongeza ya muda ya kutekeleza miradi hiyo hivyo wakandarasi wahakikishe miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula, amesema ujenzi wa soko la samaki Mkuyuni utakapokamilika wafanyabiashara zaidi ya 800 wataweza kufanya shughuli zao kwa wakati mmoja.
Naye Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Manusura Lusigaliye, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwakutoa fedha kwaajili ya kujenga soko kubwa la kisasa ambalo litafungua fursa za kiuchumi.
“Soko hili litawakusanya wafanyabiashara wengi na litachochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hivyo sisi kama Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela tunamshukuru sana sana Rais wetu kwakuendelea kutupa fedha, na tunamuombea kwa mwenyezi Mungu azidi kumpa maisha marefu ili Ilemela izidi kunufaika zaidi”, amesema Manusura.