Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF) umeshinda tuzo ya Usimamizi na Uratibu wa Hifadhi ya Jamii
kwa Sekta Binafsi nchini, wakati wa kilele cha Maonesho ya Saba ya
Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika kwenye uwanja wa EPZ
Bombambili, mkoani Geita. Tuzo hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kupokelewa na
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba wakati wa ufungaji wa
maonesho hayo.
Aidha, NSSF imeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza
katika kundi la Hifadhi ya Jamii na Huduma za Bima zilizotolewa Oktoba
12, 2024 na Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, wakati wa maonesho
hayo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Bw. Mshomba
amesema utoaji wa huduma kidijitali umekuwa nyenzo muhimu katika
kuhakikisha huduma za NSSF zinawafikia wanachama popote walipo, ikiwemo
kufungua madai ya kuomba mafao mbalimbali.
Bw. Mshomba amewataka
waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanasajili wafanyakazi wao NSSF
pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati, kwani hilo ni takwa la sheria
na vilevile kuwezesha Mfuko kuendelea kukua na kutoa huduma bora.
Aidha,
Bw. Mshomba ametoa rai kwa watu waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo
rasmi wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, baba lishe,
boda boda, wavuvi, wakulima, wafugaji na wajasiriamali mbalimbali
kujiunga na kuchangia NSSF kwa sababu ndiyo njia sahihi ya kupunguza
umasikini wa kipato na kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.
Naye,
Bw. Omary Mziya, Mkurugenzi wa Uendeshaji, amesema Mfuko utaendelea
kutoa huduma bora kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA ambapo hivi
sasa wanachama wanaweza kufungua madai yao kwa njia ya kidijitali bila
ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.
Kwa upande wake,
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele amesema
kupitia maonesho hayo Mfuko ulifikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa
makundi mbalimbali yakiwemo ya wachimbaji wadogo wa madini pamoja na
wajasiriamali zaidi 1500 Wilayani Bukombe. “Maonesho ya madini yalikuwa
fursa kwa NSSF kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha
wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi, tutoa elimu kuhusu huduma za
kidijitali pamoja na fursa za nyumba na viwanja,” amesema Bi. Lulu.
Awali,
Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Bi. Winniel Lusingu amesema katika mwaka
wa fedha 2024/25, Ofisi ya Mkoa huo imeweka lengo la kukisanya shilingi
bilioni 104 na kuwa mwaka wa fedha uliomalizika walikusanya shilingi
bilioni 64. Ameshukuru ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa uomgozi
wa Mkoa huo, Waajiri, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa NSSF.