Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt.Suleiman Jaffo amewataka wafanyabiashara kutoka Tanzania na Iran kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kupata manufaa makubwa katika masuala ya Biashara na uwekezaji.
Dkt Jaffo ametoa kauli hiyo Jijini Dar es mapema leo Octoba 16, 2024 wakati akifungua Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Iran ambalo limelenga kutengeneza mashirikiano katika sekta mbalimbali sambamba na kutafuta masoko na elimu.
Dkt. Jaffo amesema wafanyabiashara hao wakishirikiana kwa pamoja nchi hizo zitakuwa na maendeleo makubwa katika upande wa kiuchumi licha ya kuwa na historia ya muda mrefu ya mahusiano ya kidemokrasia .
“Miongoni mwa jambo linalofanyika kwa Sasa ni kuwa na Jukwaa kama hili ambalo tutaweza kubadilishana mawazo wafanyabiashara na watumishi wa Serikali na hatimaye nchi hizi mbili zinakuwa na maendeleo ya kiuchumi “amesema Dkt Jaffo
Amesema nchi ya Tanzania inauwanda mkubwa wa rasilimali katika ardhi, utalii, madini na gesi hivyo kupitia Jukwaa hilo litaweza kutoa fursa ya wafanyabiashara wa Tanzania na Iran kubadilishana mawazo na kuona sehemu gani kuna fursa hili waweze kuzitumia.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara..kama mnavyofahamu kwamba kupitia Kituo Cha uwekezaji Tanzania (TIC) mtu anaweza kufanya usajili wa uwekezaji moja kwa moja lakini sio hivyo tu kwamba uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya sekta ya gesi, Barabara, reli hii inawawezesha wafanyabiashara wengi mbalimbali waweze kufika Tanzania na kupunguza gharama za uzalishaji katika nchi yetu”amesema Jaffo
Aliendelea kueleza kuwa hivyo jukumu la Serikali kuhakikisha inawahakikishia wawekezaji wote na wafanyabiashara kwamba Tanzania Iko mbele kabisa kuhakikisha kwamba inaweka mazingira wezeshi na kusaidia wawekezaji wote kwa kuhakikisha wanafanya uwekezaji mkubwa na wafanyabiashara huku lengo likiwa kuongeza uhalali wa kibiashara katika nchi ya Tanzania.
Aidha amesema kwa upande wa mifugoTanzania inabahati kubwa ya kuwa wanyama wengi hasa katika upande wa ngombe, mbuzi na kondoo hivyo hiyo fursa kubwa kwa watanzania kupanua upande wa soko hilo katika nchi mbalimbali.
“Natoa wito kwa Watanzania na wafanyabiashara wote kuchangamkia fursa hiyo na kuhakikisha mifugo wanaifuga katika mikoa mbalimbali,”amesema na kuongeza
“Kinachotakiwa kwa sasa tuweke utaratibu mzuri wa kufanya biashara kwa lengo kubwa la kwamba mifugo hii iweze kuleta thamani kwa wananchi na kufanya biashara katika nchi ya Iran”amesema
Aidha amesema hivi karibuni Rais Dkt Samia alianzisha Tume maalumu ya Rais kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Kodi za ndani na nje na kueleza hiyo inakwenda kutoa majawabu ya uwekezaji wa aina mbalimbali ya kibiashara katika nchi Tanzania.
“Kwahiyo ndo maana nasema tunawakaribisha wawekezaji wote na wafanyabiashara waje kushiriki na watanzania katika eneo hili…kwa sababu hivi sasa Tanzania imetegeneza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na hasa dhamira ya Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha nchi hii inashirikiana na nchi nyingine na wadau wengine katika kukuza biashara baina ya nchi hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya wafanyabiashara, wenye Kilimo, Viwanda pamoja na Biashara (TCCIA) Oscar Kissanga amesema Jukwaa hilo
limewakutanisha wafanyabiashara kutoka katika sekta mbalimbali ya ikiwemo Kilimo, Madini, Mifugo ili waweze kukutana na wafanyabiashara kutoka nchini Iran.
“Lengo la Jukwaa hili ni kutengeneza mashirikiano katika sekta hizo sambamba na kutafuta masoko na elimu…wezentu Iran wanateknolojia ya hali ya juu hivyo kupitia Jukwaa hili wataweza kubadilishana uzoefu katika kutumia biashara kama nguzo ya kuwakutanisha pamoja”amesema Kissanga
Kissanga amesema kazi kubwa ya TCCIA ni kuwauganisha na kuwatafuta wafanyabiashara kutoka katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara
“Sisi TCCIA ndio tunatoa cheti cha uhalisia unapotaka kusafirishia bidhaa zako zote nje mfano parachichi, madini ni lazima upate cheti cha uhalisia kutoka kwetu..hivyo kupitia Jukwaa hili wafanyabiashara watapata elimu juu ya umuhimu wa cheti cha uhalisia pale wanaposafirisha bidhaa zao ,”amesema Kissanga
Naye Balozi wa Iran nchini Tanzania,Hossein Alvandi amesema kupitia jukwaa hilo wataweza kuwekeza katika sekta ya Kilimo,Madini na Ufugaji.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa eneo zuri la uwekezaji na maendeleo katika Afrika Mashariki na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC.
“Hii ni nafasi nzuri kwa uwekezaji wa ndani na wa nje hivyo kupitia jukwaa hilo ni eneo zuri la kujenga mtandao wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili,”amesema