Na Farida Mangube
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesisitiza umuhimu wa kuanzisha mijadala ya kitaifa inayolenga kujadili muundo wa sekta ya kilimo nchini, hasa kwa lengo la kuwashirikisha vijana kwa kiwango kikubwa zaidi katika shughuli za kilimo.
Mhe. Bashe amesema kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuendesha mijadala hiyo, kwani chuo hicho kimekuwa kitovu cha wataalamu wa kilimo. Aliongeza kuwa vijana zaidi ya 200 wanaohusishwa katika mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT) wameanza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kupitia ushiriki wao.
“Vijana hawa tunawatazama kwa matumaini makubwa kutokana na mafanikio tuliyoyaona. Tuna mpango wa kuwapa nafasi ya kusambaza mbegu na pembejeo kwa wakulima, kwani wameonesha uaminifu mkubwa kwa serikali,” alisema Mhe. Bashe.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA, Prof. Raphael Chibunda, aliiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zinazohusu bioteknolojia, hususan mbegu za GMO, ili kuwapa watafiti uhuru zaidi wa kufanya tafiti zao bila vikwazo.
“Kwa sasa, sheria za mazingira zinasema kuwa endapo kutatokea tatizo lolote linalosababishwa na mbegu za GMO, mtafiti atawajibika moja kwa moja. Hali hii inakatisha tamaa watafiti wetu,” alisema Prof. Chibunda.
Aidha, Mhandisi Tito Edimund, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vijana Kilimo Biashara wilayani Mvomero, alimwomba Mhe. Bashe kuweka mipango ya kuwawezesha vijana ambao hawapo kwenye mpango wa BBT, ili waweze kushiriki katika kilimo chenye tija kwa msaada wa kifedha kutoka serikali.