NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka ametimiza haki yake ya msingi ya kwenda kujiandikisha katika daftari la makazi la kupiga kura katika kituo cha mkoani ‘A’ pamoja na kufanya zoezi la kuwahamasisha wananchi pamoja na makundi mbali mbali kuweza kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha.
Mama Koka amesema kwamba ameamua kujiandikisha katika daftari la makazi la mpiga kura ikiwa ni kuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliweza kuzindua na kujitokeza kujiandikisha katika siku ya kwanza pindi zoezi hilo lilipoanza rasmi siku saba zilizopita.
Mama Koka ambaye pia ni mlezi wa Jumuiya ya umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha ameweza kuambatana na viongozi mbali mbali wa chama ameweza kupita katika maeneo mbali mbali katika kata ya Tumbi pamoja na Kata ya Mkuza ambapo ameweza kupata fursa ya kuzungumza na wananchi mbali mbali kwa lengo la kuweza kuwahamasisha wananchi hao ikiwa sambamba na kujionea mwenendo mzima unavyokwenda.
“Nimeweza kushiriki katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la makazi la mpiga kura ili niweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu nchi nzima na kwamba kupiga kura ni haki yangu ya msingi hivyo nimetimiza jukumu langu la kikatiba,”alisema Mama Koka.
Aidha Mama Koka aliweza kutembelea makundi mbalimbali katika kufanya hamasa ikiwemo kutembelea vijana, kuzungumza na wazee, makundi ya wakinamama ambao amewahimiza kwa pamoja kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kujiandikisha katika daftari hilo ambalo litawapa fursa ya kuweza kupiga kura.
Nao baadhi wa wananchi ambao wametembelewa na Mama Koka hawakusita kumpongeza kwa dhati kwa kuamua kufanya ziara ya kuwatembelea na kuwapa elimu na hamasa umuhimu ya kujiandikisha katika daftari hilo ikiwa sambamba na kugombea katika nafasi mbali mbali za uongozi wa serikali za mitaa.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu hivyo wananchi wote wanapaswa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kujiandikisha katika daftari la makazi ambapo linatarajiwa kufikia tamati octoba 20 mwaka huu.