Jeshi la Polisi mkoa wa Mara limefanikiwa kuteketeza zaidi ya hekta kumi za mimea inayoaminika kuwa ni bangi katika kijiji cha Magatini, wilaya ya Serengeti.
Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 17 Oktoba 2024 akiwa eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Thomas Mapuli, alisema mashamba hayo yamekamatwa kutokana na operesheni kali inayoendelea mkoani humo. Operesheni hiyo imelenga kutokomeza mtandao wa watuhumiwa wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kamanda Mapuli alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na operesheni za mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa shughuli haramu kama hizi zinakomeshwa kabisa.
Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaathiri afya za vijana na kuhatarisha amani ya jamii.