Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amefanya ziara wilayani Serengeti kufuatilia zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku zilizobaki kujiandikisha ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
Akizungumza na wananchi kwenye vituo vya Marasomoche na Majimoto, Mhe. Mtambi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, na pia kushiriki kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao.
“Tuitumie fursa hii ya kikatiba vizuri kuwachagua viongozi bora watakaosimamia miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zetu kwenye maeneo yetu,” alisema Mhe. Mtambi.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi wa Serengeti kwa mwitikio wao mkubwa katika zoezi la uandikishaji, akionesha matumaini yake kuwa Wilaya hiyo itafanya vizuri zaidi hadi kukamilika kwa zoezi hilo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, na maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa lilianza tarehe 11 Oktoba 2024, na linatarajiwa kukamilika tarehe 20 Oktoba 2024. Uchaguzi wenyewe umepangwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.