Na Said Mwishehe,Michuzi TV
SHIRIKA la Viwango Tanzania(TBS) limesema kuwa kuna juhudi mbalimbali zinafanywa kuhakikisha rangi ya risasi inatengwa na miongoni mwa jitihada hizo ni uidhinishaji wa tukio la kimataifa linalojulikana kama Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Utoaji Sumu (ILPPW) kwa ajili ya kuongeza uelewa juu ya uondoaji wa rangi ya risasi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina iliyoandaliwa na wadau wakiwemo TBS, AGENDA, na LEEP kwa lengo la kujadiliana na kuweka mikakati ya kutokomeza rangi ya risasi Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dk.Ashura Katunzi amesema juhudi za wadau hao zimewaunganisha na kukutana kubadilishana ujuzi sambamba na kushirikiana ipasavyo ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na rangi ya risasi.
“Nimefahamishwa warsha hii inalenga kuimarisha juhudi za ushirikiano wa kitaifa kwenye ramani ya kutokomeza rangi ya risasi nchini Tanzania, na inaaminika kuwa ushiriki wanu unaonyesha dhamira ya dhati katika suala hili. Uwepo wa risasi una anuwai ya athari mbaya na msisitizo zaidi juu ya athari kwa watoto.
” WHO imetambua madini ya risasi kuwa mojawapo ya kemikali 10 za masuala ya afya ya umma zinazohitaji kuchukuliwa hatua na nchi Wanachama ili kulinda afya ya wafanyakazi, watoto na wanawake walio katika umri wa uzazi. Katika suala hilo, nchi wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania zina wajibu wa kukomesha sumu ya risasi.
“Leo, waliokusanyika katika chumba hiki ni wawakilishi wa washika dau – serikali, watengenezaji wa rangi, waagizaji, wauzaji bidhaa nje, Asasi za kiraia, wasomi na watafiti, vyombo vya habari, na watumiaji ambao ni sehemu ya wajibu huo. Kila mmoja ana sehemu yake.”
Amesema kuwa miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania, ni kuidhinisha viwango vya kisheria vinavyoweka ukomo wa madini ya risasi katika rangi na mipako mingine.
Ameongeza kuwa Watengenezaji wanatakiwa kuzingatia kikomo hicho ambacho si zaidi ya sehemu 90 kwa jumla ya risasi milioni (ppm) (jumla ya risasi 90 mg/kg). Ukomo huo pia umeanishwa ndani ya nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesisitiza kwamba kwa kufanya hivyo, Tanzania imekuwa miongoni mwa asilimia 48 ya nchi ambazo zimethibitisha kuwa na udhibiti wa kisheria wa uzalishaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya rangi za risasi.
“Hata hivyo, kuwa na viwango vya kisheria vya rangi ya risasi ni hatua kuelekea kutimiza lengo. Utekelezaji wa kutosha na ufahamu miongoni mwa umma ni miongoni mwa hatua muhimu za kufikia lengo.Nawapongeza kwa kujitolea kwenu katika mpango huu hapa Tanzania ambao ninaamini unatoa mchango mkubwa katika mipango ya kimataifa ya kuondoa madini ya risasi katika rangi,”amesema Dk.Katunzi.
Kwa upande wake Dora Swai ambaye ni Ofisa programu mwandamizi wa Shirika la Agenda kwa Mazingira na Maendeleo Endelevu (AGENDA), amesema madini ya risasi ni yanatambulikana kuwa sumu inayoathiri mfumo wa fahamu.
“Kuharibu kwake maendeleo na makuzi ya mfumo huo, uwezo wa kufikiri na kupambanua mambo kwa watoto ndiyo athari kuwa inayosababisha.
“Watoto wadogo ndiyo wanaoathirika zaidi hata kwa kiwango kidogo tu cha madini hayo. Kwa mujibu wa Swai, kuacha rangi zenye risasi kuingia nchini au kuzalishwa kunabeba hatari kubwa kwa watoto ambao ni wahasiriwa wakuu wa sumu hiyo.
“Rangi zinazofungwa na viongeza vya risasi zinabeba hatari za kiafya kutokana na sumu na uchafuzi wa mazingira. Risasi inaweza kuwa na athari za kudumu kwa afya ya watoto, lakini pia inasababisha madhara kwa watu wazima,” amesema Swai.
Wakati huo huo Meneja Programu wa Mradi wa Kutokomeza Ufichuzi (LEEP), Dk. Scott Matafwalli pamoja na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bw. Yohana Nanai Goshashy Wametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina hatua zinachokuliwa kutokomeza rangi ya risasi.