WATAFITI 111 kutoka mataifa kumi ulimwenguni wamekutana katika kongamano la Elimu lililoandaliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti zao mbalimbali walizozifanya kuhusiana na elimu msingi na kutoa mapendekezo namna ya kuikuza elimu hiyo nchini.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo Dkt. Wilson Mahera, akimuwakilisha Waziri wa wizara hiyo Prof. Adolf Mkenda, amesema mada zinazowakutanisha watafiti hawa ni muhimu na zijadiliwe kwa kina kwani zinaendana na malengo ya sasa ya nchi yetu hivyo maarifa yatakayotolewa na mijadala hii yafikishwe wizarani ili kuona namna bora ya kuweza kuyatumia katika kuboresha juhudi zinazofanyika.
“Kuna mapitio makubwa katika sera na mitaala ya elimu nchini, ambapo elimu msingi inachukuliwa kama nguzo muhimu ya kuandaa watoto kuwa na uwezo wa kuwa na fikra tunduizi, mbunifu na maadili ya Kitanzania. Hivyo, kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, wataalam hawa watawasilisha machapisho yao na kuweza kujadili namna gani bora elimu msingi inaweza kutekelezwa vizuri,” amesisitiza Dkt. Mahera.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema chuo hiki kimekuwa ni nguzo muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu ya msingi nchini kwani kimekuwa kikitoa mafunzo ya stashahada ya elimu ya msingi tangu mwaka 2008 ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika ngazi hiyo.
“Pia kongamano hili ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka Thelathini ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, chuo hiki kimekuwa mbele katika kuendeleza na kuimarisha elimu ya msingi. Baada ya kuanzishwa shule za sekondari nyingi kwenye kata, walimu wenye stashahada walihamishwa kufundisha sekondari hivyo tulianzisha stashahada ya elimu ya msingi na hata walimu waliomaliza stashahada hiyo walibaki kufundisha shule hizo wakiwa na maarifa bora zaidi,” amesema Prof. Bisanda.
Dkt. Janeth Kigobe, Mhadhiri Mwandamizi na Katibu wa kongamano hilo la kimataifa, amesema kumekuwa na haja ya kujadili elimu msingi na kuweka mikakati namna ya kushawishi serikali mbalimbali duniani hususani Tanzania namna ya kukuza elimu msingi kwa manufaa makubwa ya maendeleo ya nchi yetu.
Kabla ya kongamano hilo, kulitanguliwa na matembezi ya hisani yaliyofanyika alfajiri ya Oktoba 16, 2024 katika kitongoji cha Kwamfipa mjini Kibaha ambayo yalilenga kuhamasisha umma kuhusiana na umuhimu wa elimu msingi nchini.
Kongamano hilo lenye ujumbe wa “Uboreshaji wa Elimu Msingi kwa Maendeleo Endelevu” linafanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwl. Nyerere, Kibaha Mjini mkoani Pwani kuanzia Oktoba 16, 2024 na linatarajiwa kumalizika Oktoba 18, 2024 ambapo wanazuoni kutoka nchi za Uganda, Zambia, Jamaica, Uswisi, Uholanzi, Jamhuri ya Kongo, Nigeria, Kenya, na wenyeji Tanzania Bara na Zanzibar watakutana kwa pamoja kujadili mustakabali wa elimu msingi.