NA WILLIUM PAUL, HAI.
WATU 14 wamefariki Dunia na wengine kujeruhiwa baada ya gari aina ya Costa walilokuwa wakisafiria kutoka Moshi kwenda Arusha kugongana na lori la mizigo eneo la mto kikavu wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, Nurdin Babu alisema kuwa, ajali hiyo imetoa usiku wa kuamkia Oktoba 19 mwaka huu ambapo gari ya abiria aina ya Costa ikitokea Moshi kwenda Arusha iligongana na lori la mizigo.
Babu alisema kuwa, katika ajali hiyo watu sita walifariki Dunia pale pale na wengine nane walifariki wakiwa njia kukimbizwa hospitali huku majeruhi wengine wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Hai na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya KCMC.
“Serikali ya mkoa tunasikitika sana kupoteza nguvu kazi ya watu 14 ambao walikuwa wanaenda kwenye shughuli zao na nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu wote waliopoteza wapendwa wao lakini tunazidi kuwaombea Majeruhi wote wapone haraka na kuendelea na shughuli zao” Alisema Babu.