Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Oktoba 19, 2024
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, ameeleza zoezi la uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura mkoani humo linaendelea vizuri, zoezi ambalo lilianza rasmi oktoba 11 na litakamilika Oktoba 20 mwaka huu.
Aidha amewataka ,wananchi kutumia siku moja iliyosalia kujitokeza kujiandikisha ili kutimiza haki yao ya msingi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.
Akiwa wilayani Kisarawe, Kunenge alisisitiza umuhimu wa vijana, wajasiriamali, wafanyabiashara wanawake, na makundi maalum kujiandikisha, kwani kura yao ina nguvu ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Kunenge alisema, maendeleo yanaanzia kwenye jamii, na msingi bora wa maendeleo hujengwa kuanzia ngazi za chini, na kuongeza viongozi wa ngazi ya awali ni wale wanaochaguliwa na wananchi waliojiandikisha.
Baadhi ya wananchi wa Mloganzila, kata ya Kiluvya, wilayani Kisarawe, wakiwemo Faudhia Ally, Jackson Paul, na Zawadi Ahmed, waliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwa na utaratibu wa pamoja wa kitaifa kwa zoezi kama hilo, ili kuepusha mkanganyiko unaosababishwa na maeneo mengine kuchelewa kuanza kwa ratiba.
Katika Wilaya ya Kibaha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema zoezi hilo linaendelea vizuri katika kata zote.
Alihamasisha wananchi kujitokeza zaidi ili kufikia malengo ya uandikishaji.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tumbi, Msemakweli Kalia, alifafanua kuwa hamasa ni kubwa, ingawa alisisitiza kuwa uandikishaji huu ni wa daftari la wapiga kura, na si vitambulisho vya kupigia kura.
Mkoa wa Pwani unatarajia kuandikisha zaidi ya watu milioni 1.2 kwenye daftari la wapiga kura, Uandikishaji unafanyika katika vituo 2,374 vilivyopo kwenye vitongoji 2,028, vijiji 417, na mitaa 73.