Wahitimu wa mitihani ya kitaaluma ya Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB) wametakiwa kujiendeleza kitaaluma katika nyanja mbalimbali pamoja na kuzingatia maadili ya utendaji kazi, jambo ambalo litaongeza ufanisi kwa maslahi ya taifa.
Akizungumza katika Mahafali ya 13 ya wahitimu wa mitihani ya kitaaluma ya PSPTB, yaliyofanyika leo, Oktoba 19, 2024, katika Ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande, alisema ni muhimu kwa wahitimu kuendelea kujifunza ili kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma na kuboresha utendaji kazi.
Mhe. Chande alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili katika taaluma, akiwataka wahitimu kuepuka tabia za wivu, choyo, na husuda ambazo zinaharibu utendaji wa kazi. Pia aliwahimiza kuishi vizuri na watu katika mazingira ya kazi, kuendeleza ushirikiano na kuimarisha uhusiano wa kitaaluma na nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mwenyekiti wa Bodi ya PSPTB, Bw. Jacob Kibona, alisema kuwa wahitimu hao ni rasilimali muhimu katika kusimamia na kukagua ununuzi na ugavi kwa kushirikiana na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha, Ofisi za Ukaguzi wa Ndani, mamlaka za umma, na wadau wa sekta binafsi.
Bw. Kibona aliwapongeza wahitimu waliotunukiwa vyeti katika ngazi tatu za taaluma, akisisitiza umuhimu wa kutekeleza kazi kwa kuzingatia maadili ili kulinda heshima ya taaluma na kuleta ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya taifa.