Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma Elizaberth Gumbo akieleza kuhusu zoezi kujiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.
……………
Na Muhidin Amri, Songea.
WANANCHI 83,692 sawa na asilimia 79.9 wamejiandikisha kwenye Daftari la orodha la wapiga kura katika Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma hadi tarehe 18 Oktoba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Elizabeth Gumbo alisema,kati yao wanaume 41,016 na wanawake 42,676 huku idadi ya watau ikitarajia kuongozeka siku mbili zilizobaki kabla ya kuhitimishwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura tarehe 20 mwezi huu.
Alisema,lengo la Halmashauri hiyo ni kuandikisha watu 104,698 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kutokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,lakini idadi hiyo itaongezeka kutokana na uhamasishaji mkubwa unaoendelea katika maeneo mbalimbali.
Gumbo,ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajajiandikisha kwenda kujiandikisha ili kupata haki ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi wa vitongoji na vijiji kwenye maeneo yao.
“Katika zoezi hili changamoto kubwa ni uelewa wa wananchi kuchanganya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu,wengi wanategemea kuwa wakijiandikisha watapata vitambulisho vya mpiga kura,napenda kuwafahamisha wananchi kuwa haya ni mazoezi mawili tofauti”alisema Gumbo.
Kwa mujibu wa Gumbo, mwaka 2024 unafanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa na katika zoezi hilo Serikali inaandikisha wakazi waliopo kwenye kitongoji husika hivyo wananchi wanatakiwa wawepo kwenye Daftrai la orodha ya mpiga kura.
Alieleza kuwa,Daftari hilo litatumika kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa tu utakaofanyika tarehe 27 Mwezi ujao na vitambulisho wanavyoulizia vitatolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Alisema,wananchi watakojiandikisha katika Daftari la orodha la wapiga kura ndiyo watakaopata fursa ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wao katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Gumbo,amewataka watendaji wa vijiji na kata kuendelea kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili waweze kujitokeza kujiandikisha ili kufikisha lengo la kuandikisha wananchi 104,698 katika Halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine,Gumbo amefanya kikao na wadau wa vyama vya siasa kwa lengo la kujadili maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo amewataka wadau hao kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa haki,amani na utulivu.
Aidha alisema,idadi ya vitongoji katika Halmashauri hiyo itabaki 443 na mabadiliko yatakuwa ni kuongezeka kwa vituo vya kujiandikisha na kupiga kura ambavyo vitakuwa 453.
Alisema,lengo la kuongeza vituo hivyo ni kurahisisha huduma kwa wananchi ili wasilamike kutembea umbali mrefu kwenda kwenye vituo vya kupiga kura.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kazi kubwa anayoifanya kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la mpiga kura.
Mhagama ambaye ni Waziri wa afya,amewataka wananchi wa jimbo la Peramiho ambao bado hawajajiandikisha kutumia siku chache zilizobaki kwenda kujiandikisha ili waweze kupata fursa ya kuchagua viongozi wao wa vitongoji na vijiji kwenye uchaguzi unaoatarajia kufanyika mwezi ujao.