Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Andrew Mbunda akizungumzia zoezi la uandikishaji katika Daftari la wapiga kura.
Jengo la Utawala la Halmashauri ya wilaya Mbinga ambalo limezinduliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alipokuwa kwenye ziara ya siku saba mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi Maalum, Mbinga
…………
WATUMISHI wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wamelazimika kutoka ofisini na kwenda kupiga kambi katika vijiji mbalimbali ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la wapiga kura.
Halmashauri hiyo imefikia uamuzi huo ili kuhakikisha hakuna mwananchi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anakosa nafasi ya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Andrew Mbunda wakati akikagua zoezi la uandikishaji wapiga kura katika vituo mbalimbali wilayani humo.
Alisema,zoezi la uandikishaji wapiga kura linakwenda vizuri na kuna mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza na hadi sasa zaidi ya asilimia 92 ya wamejiandikisha katika vituo 782 vilivyotengwa katika Halmashauri hiyo.
Mbunda alisema,mwitikio huo umetokana na wananchi kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kujiandikisha na uhamasishaji unaofanywa na watumishi wa ngazi mbalimbali za Halmashauri wakiwemo watendaji wa vijiji na kata na matangazo yanayotolewa kila siku kwenye vijiji na vitongoji.
Alisema,ili kufikisha lengo la asilimia 100 la uandikishaji na kupata takwimu sahihi za wapiga kura katika uchaguzi huo,Halmashauri imeweka utaratibu ambapo kila kitongoji,kijiji na kata zenye jukumu la kutambua wakazi wake na wale wenye sifa wanahamasishwa kwenda kujiandikisha ili waweze kushiriki katika uchaguzi huo.
“Tumebakiwa na siku moja kabla ya kufunga zoezi la uandikishaji,tunaamini asilimia 8 iliyobaki tutaifikia kutokana na mikakati kabambe tuliyojiwekea katika Halmashauri yetu,tumeongeza nguvu ili kuwafikia watu wote wenye sifa ya kupiga kura siku ya tarehe 27 mwezi ujao”alisema Mbunda.
Pia alisema,katika utekelezaji wa zoezi hilo changamoto kubwa ilikuwa uelewa mdogo wa wananchi kwani siyo wote waliotambua umuhimu wa kujiandikisha na kupiga kura.
Kwa mujibu wa Mbunda ni kwamba,awali wananchi walidhani wakifika kwenye vituo watatumia muda mrefu kujiandikisha,lakini wanapofika kwenye vituo wanakuta hali ni tofauti kwani wanatumia muda mchache, hivyo wale ambao hawajajiandikisha wanakwenda kwenye vituo vilivyotengwa.
“Hofu kubwa ya wananchi walidhani wakifika watapoteza muda wao wa siku nzima wakiwa vituoni,kumbe hali ni tofauti kabisa kwani ukifika kituoni mwandikishaji atakuuliza majina matatu,umri na kusaini kwa kidole gumba au kwa peni tu na siyo vinginevyo”alisema Mbunda.
Mbunda,Namevishukuru vyama vyote vya siasa kwa kazi nzuri ya kuhamasisha wanachama wao kwenda kujiandikisha na kuwaomba waendelee na uhamasishaji huo hadi siku ya kupiga kura tarehe 27 mwezi Novemba mwaka huu.
Ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajajiandikisha kutumia siku chache zilizobaki kwenda kujiandikisha ili kupata fursa ya kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo katika vijiji vyao.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga Ambrose Kapinga alisema,amefurahishwa na zoezi la uandikishaji linavyoendelea kwani wanapofika kwenye vituo wanatumia muda mfupi na hivyo kuwapa nafasi kwenda kushiriki shughuli nyingine za kujiletea maendeleo.
Anna Komba mkazi wa Kiamili,ameipongeza Serikali kwa kuandaa uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao utawezesha kuwapata viongozi bora watakaoshirikiana nao kuleta maendeleo kwenye vijiji vyao.