Na Mwandishi Wetu
Serikali inafanya mazungumzo na kampuni ya China Overseas Engineering Group Co. Ltd. (COVEC) ambayo imeonesha nia kuwekeza Dola za Marekani bilioni 1 (zaidi ya Shilingi trilioni 2.7) kujenga barabara zenye lengo la kupunguza kero ya foleni jijini Dar es Salaam.
Kampuni hiyo ya COVEC inataka kutekeleza mradi huo wa kimkakati kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha PPP, David Kafulila, amesema kuwa mwekezaji huyo tayari amefanya kazi za awali, kama vile upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi (preliminary feasibility study).
Kampuni ya COVEC sasa inataka kuingia katika Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU) na Serikali ili iweze kufanya upembuzi yakinifu kamili (full feasibility study) ya mradi huo, kwa mujibu wa Kafulila.
“Utafiti uliofanywa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) mwaka 2020 umebaini kuwa biashara hupoteza asilimia 20 za faida zao kutokana na foleni za magari kwenye barabara za Dar es Salaam,” Kafulila amesema.
Dar es Salaam ni moja ya miji inayokuwa kwa kasi zaidi barani Afrika na hivyo kukumbwa na kero kubwa ya foleni, hususan nyakati za asubuhi na jioni.
Serikali imekuwa inachukua hatua kadhaa kukabiliana na foleni jijini Dar es Salaam, ambayo ndiyo kitovu cha uchumi wa Tanzania.
Jitihada hizi ni pamoja na ujenzi wa daraja za juu (flyovers) na ujenzi wa Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (BRT) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kwa mujibu wa Kafulila, kampuni ya COVEC inataka kujenga barabara 10 za mazunguko (ring roads) kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.
Barabara hizo za mazunguko ni pamoja na barabara 6 za ndani (inner ring roads) na barabara 4 za nje (outer ring roads).
Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kunatarajiwa kupunguza foleni kwenye barabara kuu za Dar es Salaam, kwani magari yataweza kutumia barabara za kuzunguka zenye malipo (toll roads).
Kampuni ya COVEC ya China ina uzoefu wa kujenga miradi ya miundombinu mikubwa na ya saizi ya kati kwenye takribani nchi 100 duniani, yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 12.22.
Miradi iliyotelekezwa na kampuni hiyo inayomilikiwa na Serikali ya China ni pamoja na ujenzi wa barabara, nyumba, madaraja, miradi ya maji, umeme na sekta nyingine.