Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Shule Kuu ya Elimu kimejipanga vyema kuhakikisha miundombinu ya ufundishaji inakuwa rafiki kwa wanafunzi mkondo wa amali katika shule ya Sekondari Mafiga ili wanawajengea uwezo wanafunzi hao.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Jamal Jumanne kwenye mahafali ya 15 ya shule hiyo, amesema lengo kuu la Elimu ya Amali ni kukuza ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja katika mazingira halisi ya kazi au maisha.
Dkt. Benedicto Msangya ni Mratibu wa Shule ya Sekondari Mafiga kutoka SUA amesema kwa sasa shule hiyo inafundisha Mkondo wa Amali wa Kilimo ukiwa umegawanywa katika makundi matatu ambayo ni uzalishaji wa mazao, kilimo cha bustani na mbogamboga pamoja na uzalishaji wa wanyama pamoja na afya zao.
Katika hatua ya awali wanafunzi wataweza kupata mafunzo kwa vitendo SUA ambapo itawasaidia watakapomaliza shule ya sekondari waweze kujiajiri na wale watakao kwenda kwenye ngazi ya juu waweze kuwa wanafunzi bora na hivyo kuweza kulitumikia taifa.
Daniel Kavula ni Mwalimu wa wanafunzi wa Amali shule ya Sekondari Mafiga anasema Mkondo wa Amali umepokelewa vizuri na wanafunzi pamoja na wazazi kwani mpaka sasa wameandikisha wanafunzi 57.
Anasema mkondo huu wa amali unaenda kuwa mwarobaini kwa vijana kukosa ajira na kusubiri kuajiliwa kwani kupitia ujuzi wanaoupata utawasaidia kuendana na soko la ajira na wengine kujiajili na kuajiri wengine.
Karunde Hamisi ni mmoja wa wanafunzi anasoma Elimu ya Amali shule ya Sokondari Mafiga anasema ameamua kujiunga na Elimu ya Amali ili kutimiza ndoto zake za kuwa Afisa Kilimo bila ya kupitia changamoto zozote.
Hakupata changamoto pale alipoitaarifa familia yake kuwa anatamani kujinga na Elimu ya Amali mara bada ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, Matumaini yake baada ya miaka kumi mbele atakuwa Afisa Kilimo mkubwa.
“Mama yangu alinielewa nilivyo mtaarifa nataka kujiunga na Elimu ya Amali kwani mara nyingi amekuwa akinielewa pale ninapompa vipaombele vyangu katika elimu” amesema Karunde.