Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, leo Oktoba 21, 2024, imesaini makubaliano ya uwekezaji na mafunzo na Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Kielektroniki ya China (CECIS LTD). Kupitia makubaliano hayo, zaidi ya makampuni 600 ya utengenezaji wa vifaa vya kompyuta yataweza kuwekeza nchini Tanzania.
Lengo la uwekezaji huu ni kuongeza ujuzi kwa vijana wa Kitanzania na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utengenezaji wa kompyuta duniani.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla, pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya CECIS, Guo Zhaoping, huku yakishuhudiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Maryprisca Mahundi. Mahundi alibainisha kuwa makubaliano haya ni hatua kubwa kwa Tanzania katika kuimarisha uchumi wa kidijitali.
“Makubaliano haya ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China aliyoifanya hivi karibuni. Kampuni hii ni wataalamu wa usalama wa mitandao, na hivyo wataalamu wa Kitanzania watajifunza kutoka kwao, tukizingatia hitaji la wataalamu zaidi wa TEHAMA nchini,” alisema Mahundi.
Katibu Mkuu wa Wizara, Mohammed Abdulla, alisema kuwa uwekezaji huu utatoa fursa kubwa kwa Watanzania kujifunza, kupata ajira, na kujiendeleza katika sekta ya teknolojia.
Mwenyekiti wa CECIS, Guo Zhaoping, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia wa Kamati ya Kampuni hiyo, alisema kuwa uwekezaji huu unafuata misingi ya ushirikiano wa Tanzania na China na unalenga kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
“Kampuni yetu inafanya uwekezaji katika maeneo makuu matano, ikiwemo sekta ya kompyuta na usalama wa mitandao. Tunapofanya shughuli hizi za kibiashara, pia tunalenga kukuza uchumi wa kidijitali nchini Tanzania na katika nchi nyingine,” alisema Bw. Zhaoping.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga, alisema kuwa sehemu ya makubaliano haya pia ni kuvutia makampuni mbalimbali ya kielektroniki kuwekeza nchini. Aidha, mwaka 2025 kutakuwa na maonesho makubwa ya utengenezaji wa vifaa vya kompyuta Afrika, ambapo Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume yake watakuwa wenyeji wa maonesho hayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla, na Mwenyekiti wa CECIS, Guo Zhaoping.