Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
Baraza la Taifa la mitihani (NECTA) limetangaza rasmi kuanza kwa mtihani Wa upimaji kitaifa wa darasa la nne na mtuhani wa kidato cha pili huku likitoa rai kwa wanafunzi kutojigusisha na udanganyifu kwani atakaebainika atafutiwa mitihani yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo octoba 22,2024 katibu mtendaji wa NECTA Dkt.Said Mohamed amesema mitihani hiyo inatarajiwa kuanza octoba 22 na 23,2024 kwa upimaji wa darasa la nne wakati wa kidato cha pili ukianza Octoba 28 na kumalizika Novemba 7,2024.
Amesema jumla ya wanafunzi 1,633,900 wamesajiliwa kufanya upimaji wa Kitaifa wa darasa la nne wakati wanafunzi 879,291 wamesajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili.
“Maandalizi yote kwa ajili ya upimaji wa kidato cha pili na darasa la nne yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za upimaji pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo katika Halmashauri/Manispaa zote nchini”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa maandalizi yote pia kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu yamekamilika huku akitoa rai kwa wasimamizi kuhakikisha wanafuata kanuni zote za mitihani hasa kuwaongezea muda wanafunzi hao wenye mahitaji maalum.
“Wasimamizi wahakikishe wanafunzi wenye mahitaji maalum wanafanya upimaji ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi ambapo ni pamoja na kuwapa mtihani wenye maandishi ya nukta nundu kwa wanafunzi wasiiona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu lakini pia wanafunzi wote wenye mahitaji maalum kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine”,Amesema Dkt Mohamed.
Akizungumzia umuhimu wa upimaji huo amesema matokeo ya upimaji wa darasa la nne na kidato cha pili huwezesha wadau wa elimu,walimu wa kuu wa shule na walimu kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika maeneo yanayobainima kuwapa changamoto.
Aidha ameongeza kuwa kwa wanafunzi wa kidato cha pili wa kujitegemea upimaji huo utawawezesha kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa watakao faulu upimaji huo.
Hata hivyo NECTA imetoa rai kamati za mitihani za mikoa na Halmashauri zihakikishe usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vituo hivyo vitumike kwa mujibu wa Muongozo uliotolewa na Baraza hilo.