Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi za Afrika (African Caucus – WB) uliomshirikisha Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga, Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambako Dkt. Nchemba, anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.
Mkutano huo uliwapa fursa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika kuwasilisha vipaumbele na changamoto zinazoathiri maendeleo barani Afrika kwa Rais wa Benki ya Dunia Bw. Ajay Banga, ili kuzingatiwa katika mipango na mikakati ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na nchi za Afrika. Baadhi ya changamoto zilizoainishwa ni pamoja na: fursa chache za ajira kwa vijana; miundombinu hafifu ya umeme, barabara na tehama; uzalishaji mdogo wa chakula; tishio katika uhimilivu wa madeni; na ongezeko la gharama za upatikanaji wa mikopo.
Bw. Banga alikubaliana na umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na wakutosha katika kuchochea shughuli za uchumi na namna unavyoweza kuathiri uzalishaji wa mbolea na chakula. Hivyo alibainisha kuwa Benki ya Dunia ipo tayari kusaidia utekelezaji wa miradi ya umeme ambayo inahusisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira na kuhimiza matumizi ya TEHAMA hususan kwa kundi kubwa la vijana kwa kuwa ni chanzo moja wapo kikubwa cha ajira.