Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fred Msemwa (wa kwanza kushoto) akionesha Tuzo walioshinda ya Nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (Africa Union for Housing Finance – AUHF) inayo tambuliwa na Umoja wa Afrika katika Mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika leo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam.(PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investment (WHI) Dkt. Fred Msemwa akizungumza na Waandishi wa habari leo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam kuhusu Tuzo walioshinda ya Nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (Africa Union for Housing Finance – AUHF) inayo tambuliwa na Umoja wa Afrika.
Afisa Uhusiano na Masoko Mwandamizi wa WHI Maryjane Makawia akitoa ufafanuzi wa jambo kuhusu WHI ilivyoshinda Tuzo ya Nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (Africa Union for Housing Finance – AUHF) inayo tambuliwa na Umoja wa Afrika.
Mkuu wa Idara ya Masoko na Mauzo wa WHI Raphael Mwabuponde akitoa shukrani kwa wadau mbalimbali kwa kutoa ushirikiano katika uekelezaji wa majukumu ya WHI tangu kuanzishwa kwake.
Waandishi wa habari wakiwa katika Mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa WHI Dkt. Fred Msemwa.
…….
NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Watumishi Housing Investment (WHI) imetunukiwa tuzo ya Nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (Africa Union for Housing Finance – AUHF) inayo tambuliwa na Umoja wa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa WHI Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa tuzo hiyo imetolewa katika mkutano mkuu wa AUHF mwaka huu uliofanyika Zanzibar hivi karibuni.
Dkt. Msemwa amesema kuwa tuzo hiyo ni ya heshima ambayo inatambua jukumu la WHI katika kuwezesha umiliki wa nyumba kwa watu wa kipato cha chini na kati nchini Tanzania.
“Juhudi zilizofanywa na WHI katika kuleta suluhisho la njia nafuu za malipo za nyumba ikiwemo malipo endelevu yanayolipwa kipindi cha ujenzi bila riba pamoja na utaratibu wa mpangaji mnunuzi vilitajwa kama sababu kuu za ushindi” amesema Dkt. Msemwa.
Dkt. Msemwa amesema kuwa utaratibu huo umeleta unafuu mkubwa kwa watu wanaotamani kumiliki nyumba ambazo zinauzwa kwa bei nafuu kati asilimia 10 hadi 30 ukilinganisha na bei ya soko.
Amefafanua kuwa bei za ununuzi wa nyumba WHI uanzia shilingi milioni 38 ambayo imewawezesha watanzania wengi kufikia ndoo za kumiliki nyumba.
“Tuzo imekuja wakati tunasherekea kipindi maalum kwa WHI kwani inatimiza miaka 10 ya ubunifu na uongozi katika sekta ya makazi” amesema Dkt. Msemwa.
WHI ni taasisi ya umma ambayo chini ya Ofisi ya Rais Utumishi imekuwa taasisi ya kwanza Afrika Mashariki kupokea tuzo ya heshima kwa kuibuka kinara kutoka taasisi zinazohusiana na sekta ya makazi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Tuzo za AUHF zinatambua michango thabiti ya kuendeleza sekta ya makazi barani Afrika, ushindi wa WHI umetokana na utekelezaji wake wa kipekee katika kubuni na kutekeleza miradi ya nyumba yenye gharama nafuu na hivyo kuleta unafuu kwa wanunuzi kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
AUHF ni Shirika muhimu linalounganisha wadau wa makazi barani Afrika kwa zaidi ya miaka 40 limewezesha washiriki kuendeleza ufumbuzi zaidi wa makazi ya bei nafuu.