MAWAZIRI wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola wamekutana leo Oktoba 24, 2024 kujadili na kupitisha ajenda Kuu ya Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) ya Ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ya kimaendeleo ‘One Resilient Common Future’ pamoja na agenda nyingine zitakazojadiliwa katika vikao vya Wakuu wa Nchi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo naye ameshiriki Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya, Fiamē Naomi Mataʻafa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Samoa. Mkutano huo umeridhia agenda za ustahimilivu wa mazingira, ustahimilivu wa uchumi, ustahimilivu wa watu katika jamii, na ustahimilivu wa taasisi zinazolinda demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu kuwekwa mezani kwenye mkutano wa ngazi za juu.
Mbali na Agenda hizo, Mawaziri pia wamepokea na kupitisha taarifa za Jukwaa la Wanawake, Jukwaa la Biashara, na Jukwaa la Vijana yaliyokuwa yakiendelea kwa wiki hii.
Vipaumbele vya Tanzania katika Mkutano wa CHOGM ni pamoja na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi, kuwezesha vijana na wanawake kiuchumi, kukuza matumizi ya teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji kwa nchi wanachama.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Madola unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia kesho Oktoba 25 na 26, 2024, ambapo Mheshimiwa Kombo atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.