*Mfumo ni kwa ajili ya kuchakata taarifa za fedha.
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
Tausi Africa imezindua rasmi Manka ambao ni mfumo wa uchambuzi wa kifedha unaotumia teknolojia ya Akili Mnemba(AI) uliobuniwa kuboresha tathmini za mikopo katika uchumi usio rasmi wa Tanzania.
Mfumo huu unafanyia uchambuzi taarifa za benki na fedha za simu likiwawezesha watoa huduma za kifedha kufanya maamuzi ya haraka na sahihi zaidi kuhusu mikopo ambapo inapunguza muda wa tathmini za mikopo kutoka takriban saa 3 kwa mteja hadi chini ya dakika 2, Manka inalenga kuongeza ufanisi katika sekta ya kifedha na kusaidia ujumuishaji wa kifedha.
Uzinduzi huu wa mfumo huo jijini katika katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam ukiwaleta pamoja wadau kutoka sekta ya benki na fedha ili kujadili athari zinazoweza kutokana na mfumo huu kwenye mazoea ya utoaji mikopo.
Akuzunguza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania ‘Financial Sector Deepening Tanzania (FSDT), Erick Massinda amesema, “Manka inaashiria hatua kubwa zilizopigwa kwenye tasnia ya fedha Tanzania.
Amesema kwa kutumia data na taarifa mbadala pamoja na teknolojia, mfumo huu unalenga kutatua changamoto kubwa za utoaji wa mikopo, hasa kwa watu wasio fikiwa kikamilifu na huduma za kifedha.
Massinda amesema Uwezo wa Manka wa kutoa tathmini jumuishi kuhusu uwezo wa kurejesha mkopo utaboresha upatikanaji wa fedha, na pia utawezesha ukuaji wa uchumi jumuishi.
Aidha amesema kadri Tanzania inavyoendelea kukaribisha uhuru wa kifedha (open finance), ndipo umuhimu wa ubunifu wa kitechnolojia kama Manka unaongezeka ili kuhakikisha kwamba taasisi zinazotoa huduma za fedha zinaweza kuwahudumia wateja wao kikamilifu na kusaidia kukua kwa biashara ndogo na za kati.”
Wakati wa uzinduzi huo, Tausi Africa pia ilitangaza ushirikiano wake na Credit Info Tanzania ili kupanua wigo na athari za Manka ndani ya sekta ya kifedha.
Amesema ushirikiano huu unawawezesha makampuni yote mawili kutoa uwezo wa juu wa uchambuzi wa mikopo wa Manka kwa watoa huduma za kifedha mbalimbali, hivyo kuwawezesha kuwahudumia wateja wao kwa maarifa na suluhisho bora za kifedha amba ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuboresha huduma za kifedha na kusaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Afisa Mtendaji Mkuu Credit Info Tanzania (LTD) Edwin Urasa, Tanzania, amesema ubunifu wav “Manka utaboresha kwa kiasi kikubwa jinsi ya kufanya tathmini za uwezekano wa kutokulipa mikopo katika masoko yasiyohudumiwa vya kutosha.
Urasa amesema zaidi ya tathmini ya uwezekano wa kutokulipa mkopo, Manka itawezesha benki kuongeza idadi ya wateja na kutoa fursa ya suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya kila mteja.
Amesema kwa kutumia Akili Mnemba, taasisi za kifedha zitaweza kufanya maamuzi ya uhakika yanayotokana na data kwa muda mfupi, kuhakikisha watu wengi wanapata mikopo wanayohitaji.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Derick Kazimoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Africa Technologies Limited, alisema, “Manka imeundwa ili kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa kuwawezesha watoa huduma za kifedha kuwahudumia wateja wao kwa ufanisi zaidi. Kwa kuboresha tathmini za mikopo na kutoa maarifa kuhusu tabia za wateja, Manka inaziwezesha taasisi kutoa suluhisho za kifedha haraka zaidi na kwa njia ya kibinafsi, siyo tu katika mikopo, bali pia kwenye bidhaa mbalimbali za kifedha. Zaidi ya hayo, Manka inasaidia kuwalinganisha wateja na chaguo za kifedha zinazokidhi mahitaji yao vyema zaidi, hivyo kuongeza upatikanaji wa suluhisho bora za kifedha kwenye soko.
Amesema Kipaumbele chao ni kuwawezesha watoa huduma za kifedha kukidhi mahitaji ya wateja wao, hivyo kufungua fursa kwa ujumuishaji bora wa kifedha.”
Mfumo huu unatumia Akili Mnemba kutoa uchambuzi wa kina wa hatari za mikopo na kuwatathmini awali watumiaji kutoka taasisi mbalimbali za kifedha kwa usahihi wa hali ya juu. Manka inaakisi dhamira ya Tausi ya “Kufungua upatikanaji wa fedha kwa uchumi usio rasmi wa Afrika” kwa kuchochea ujumuishaji wa kifedha na kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs).
Manka inawakilisha uwajibikaji na hekima ya kifedha, sifa zilizochochewa na jina lake kutoka kabila la Wachagga. Thamani hizi zinaakisiwa ndani ya Manka, ikitoa uchambuzi wa kifedha ulio wazi na wenye maarifa, unaowezesha maamuzi ya busara na kuweka njia ya fursa zaidi za kifedha nchini Tanzania.
Ufanisi ambao Manka inaleta kwenye tathmini za mikopo utasaidia taasisi za kifedha kuwahudumia wateja vyema zaidi huku ikipunguza hatari zinazohusiana na utoaji wa mikopo, hasa katika sekta ambazo kwa jadi hazikuhudumiwa vya kutosha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Africa Technologies Limited , Derick Kazimoto akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Manka wa uchakataji na uchambuzi wa taarifa za fedha na zinazotolewa na kampuni za simu na Taasisi za Fedha katika kutoa suluhisho ya ukopaji kwa kutumia taarifa hizo jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Credit Info Edwin Urasa akizungumza kuhusiana na ushirikiano kati ya Tausi na Credit Info kwenye mfumo wa Manka ,jijini Dar es Salaam .
Mkuu wa Teknolojia ya Ufundi (CTO) Harvey Kadyanji akizungumza kuhusiana na umhimu wa mfumo wa Manka katika Teknolojia ya sasa ,jijini Dar es Salaam.
Watendaji wa Wakuu wa TAUSI na Credit Info katika picha mara baada ya uzinduzi wa mfumo wa Manka jijini Dar es Salaam .
Mkurugenzi Mtendaji wa Tausi Africa Technologies Limited , Derick Kazimoto akiwa akizungumza akiwa na timu ya taasisi ya watenda kazi wa taasisi hiyo wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Manka jijini Dar es Salaam.