NA MAELEZO ZANZIBAR 24/10/2024
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmin katika uzinduzi wa Tamasha la Utalii na Uwekezaji linatarajiwa kufanyika Oktoba 25,2024, katika Viwanja vya Maonyesho Nyamanzi.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Karume house, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Mudrik Ramadhani Soraga amesema Tamasha hilo la kwanza kufanyika hapa Zanzibar ambalo litakuwa la kihistoria na kuitangaza Zanzibar kiutalii.
Amesema lengo la Tamasha hilo ni kuziibua fursa za utalii zilizomo ndani na nje ya nchi pamoja na kuweka mikakati madhubuti itakayoielezea Zanzibar na utalii ili kustawisha uchumi wa nchi.
Amefahamisha kuwa Tamasha hilo litashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa hoteli ambao watachangia kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyomo nchini na kupata nafasi ya kuonesha bidhaa zao pamoja na shughuli wanazozifanya.
Aidha amesema Sekta ya utalii inaendelea kuchangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la taifa na kuingiza zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni hivyo Serikali itaendelea na mkakati wa kuiendeleza sekta hiyo ili ipate tija.
Akitoa wito kwa wananchi kuwataka kujitokeza kwa wingi kwa kujionea shughuli za utalii zinavyoratibiwa pamoja na kuona namna Serikali inavyoipeleka mbele sekta ya utalii.
Zaidi ya washiriki 1,200 watarajiwa kufika katika Maonyesho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Maonyesho Nyamanzi.