SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) wanatarajiwa kusaini mkataba wa mashirikiano ili kubadilishana uzoefu na kupeana ushauri wa kitaalamu ambao utaenda kuleta matokeo chanya ya kuongeza ufanisi, uadilifu na uzalendo katika kufikia dhamira ya serikali ya uchumi endelevu.
Ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N’Hunga, wakati alipoongoza wajumbe wa kamati hiyo pamoja na viongozi wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) walipotembelea ofisi za NBAA kwa lengo la kuimarisha ushirikiano ambao utaleta tija kwenye sekta ya Uhasibu na Ukaguzi nchini.
“Mashirikiano hayo yana lengo la kuongeza mahusiano kati ya Baraza la Wawakilishi, taasisi changa ya ZIAAT na NBAA, ambayo inaratibu wahasibu, washauri elekezi wa Kodi na wakaguzi upande wa Zanzibar ili Taasisi hizi mbili zisaidiane kubadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi wa kazi,” amesema Mhe. Mihayo.
Kwa upande wake Mkurungezi Mtendaji wa Bodi ya Taifa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius Maneno ameeleza kuwa NBAA imekuwa na majukumu makubwa nchini, yakiwemo kusajili wanafunzi na wanachama, kusimamia maadili ya kitaaluma, na kuendeleza viwango vya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu.
“NBAA ni mwanachama wa Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC) na pia inashirikiana na mashirika ya Uhasibu Afrika pamoja na Afrika Mashariki kuhakikisha wanachama wake wanaweza kufanya kazi kimataifa kwa viwango vinavyokubalika”.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), CPA. Ame Burhan Shadhil, amesema kuwa taasisi hiyo changa yenye umri wa mwaka mmoja imejipanga kujifunza kutoka NBAA ambayo ni taasisi kongwe zaidi nchini na hii ni nafasi nzuri kwa taasisi yetu kujifunza kuhusu usimamizi wa wanachama na viwango vya maadili kwa wahasibu na wakaguzi ili kukuza utaalamu wetu Zanzibar.
Aidha, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mwanaasha Khamis Juma, amesema kuwa ziara hiyo inatoa fursa kwa kamati yao kujifunza ili kuboresha kanuni na sheria za Uhasibu Zanzibar na kuyachukua yale tuliyojifunza hapa NBAA ili kuboresha kanuni ambazo tayari zipo kwa ufanisi zaidi.
Mashirikiano haya yanatarajiwa kuimarisha sekta ya uhasibu na kutoa mchango muhimu katika kufanikisha azma ya serikali ya uchumi endelevu kwa kuwa na wahasibu na wakaguzi wenye viwango vya kimataifa na maadili bora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N’Hunga akizungumza wakati wajumbe wa kamati hiyo pamoja na viongozi wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) walipotembelea ofisi za NBAA kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujifunza kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo.
Mkurungezi Mtendaji wa Bodi ya Taifa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius Maneno akitoa maelezo kuhusu kazi zinazofanywa na Bodi hiyo wakati Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na viongozi wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) walipotembelea ofisi za NBAA jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), CPA. Ame Burhan Shadhil akizungumzia mashirikiano wakati Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na viongozi ZIAAT walipotembelea ofisi za NBAA kwa lengo la kuimarisha ushirikiano ambao utaleta tija kwenye sekta ya uhasibu nchini ili kuongeza ufanisi, uadilifu na uzalendo katika kufikia dhamira ya serikali.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakichangia mada
Baadhi ya Wakurugenzi wa NBAA wakiwasilisha kazi mbalimbali zinazofanywa na kurugenzi zao kwa Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na viongozi ZIAAT walipotembelea ofisi za NBAA
Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Bodi ya Taifa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) pamoja viongozi wa Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) waliotembelea NBAA.