NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kupitia kituo chake cha kudhibiti matukio ya sumu, kimewataka wazalishaji na waingizaji wa rangi nchini kuhakikisha wanazingatia maelekezo waliyopewa ili kudhibiti sumu itokanayo na madini ya risasi kwa lengo la kuzuia athari .
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 25,2024 Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa serikali Daniel Ndiyo kwenye mkutano uliowakutanisha wadau katika tasnia ya rangi ambapo umekusudia kuimarisha ushirikiano katika pande zote kwa dhumuni la kuhakikisha usalama kwa jamii.
“Rangi imekuwa ikitumika kupaka kwenye mabati ambapo watu katika kipindi cha mvua hutumia maji hayo ikiwa uhakika wa usalama wake kwa matumizi haujulikani”. Amesema
Aidha ametoa rai kwa wadau wanaohusika kwenye tasnia ya rangi,kuondokana na dhana potofu ambayo imezoeleka,kutumia maziwa pekee kwa ajili ya kudhibiti sumu mwilini kwani inaweza kudhibiti baadhi ya sumu chache pekee na sio zote Kama ilivyo zoeleka.
Kwa upande wake mdau Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalam ya Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu Prof. Amos Mwakigonja amewaagiza watu wanaoshughulika na kazi zinazohusiana na madini ya risasi kuunga juhudi zinazofanyika kwakuachana na shughuli ambazo zinahusiana na usambazaji wa madini hayo katika mazingira,ambapo itasaidia kuepusha madhara kwa watu.