Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio
akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji Tuzo kwa
Mawakala na Wadau wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania ambayo inaunga
mkono juhudi za Serikali za kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya
Nishati Safi ya Kupikia kupitia bidhaa za Puma Gas.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio
(katikati), akizungumza na Kamishna wa Petroli na Gesi, Godluck
Shirika pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy
Tanzania, Bi. Fatma Abdallah jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya
utoaji Tuzo kwa Mawakala na Wadau wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania
ambayo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuelimisha jamii kuhusu
matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia bidhaa za Puma Gas.
……………..
*Asisitiza nia ya Serikali ni kutoa huduma stahiki bila kuangalia
umbali au kipato
*Apongeza kampuni ya Puma Energy Tanzania kushirikiana na Serikali
uhamasishaji Nishati Safi ya Kupikia
*Puma Energy Tanzania yaahidi kuendeleza ushirikiano
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema
Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na miundombinu
ya Sekta ya Nishati nchini ili kuwezesha wananchi kufikiwa na huduma
stahiki bila kujali umbali na vipato vyao.
Dkt. Mataragio ameyaeleza hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla
ya utoaji Tuzo kwa Mawakala na Wadau wa Kampuni ya Puma Energy
Tanzania ambayo inaunga mkono juhudi za Serikali za kuelimisha jamii
kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia bidhaa za Puma Gas.
Dkt. Mataragio amesema moja ya majukumu ya Wizara ya Nishati ni
kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma na watumiaji ili kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali
utakaopelekea utoaji wa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni moja ya
vipaumbele vya Serikali.
Katika hafla hiyo, Dkt.Mataragio ameipongeza kampuni ya Puma kwa
jitihada zinazounga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika
kuhamasisha jamii ili itumie Nishati Safi ya Kupikia na hivyo kutimiza
lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia
ifikapo mwaka 2034.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan amekuwa Balozi na kinara katika kuhamasisha matumizi ya Nshati
Safi ya Kupikia nchini na Duniani ili kuhakikisha Watu wanaondokana
na matumizi ya kuni na mkaa ambao una madhara kwa afya na kusababisha
uharibifu wa mazingira.
Kuhusu Tuzo hizo zilizotolewa na Puma Energy Tanzania kwa Mawakala na
Wadau mbalimbali nchini, Dkt.Mataragio ameelekeza kuwa ziwe chachu ya
kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ufanisi kulingana na vigezo na
mashariti ya Kampuni kwa maslahi ya jamii.
Amesema kupitia mfano uliooneshwa na Puma Energy Tanzania wa
kuwakutanisha wadau wake kila mwaka ili kuzungumzia mafanikio na
changamoto zilizopatikana, iwe ni chachu kwa kampuni nyingine kuiga
mfano huo ambao unasaidia kukuza sekta ya Nishati nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy
Tanzania, Bi. Fatma Abdallah ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali
za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuahidi
kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuwafikishia wananchi bidhaa ya
Puma Gas kupitia kwa Mawakala na Wadau waliopo maeneo mbalimbali.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Kamishna wa Petroli na Gesi, Godluck Shirima.